Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametoa amri kwa makampuni ya udalali yanayovunja nyumba zilizojengwa katika maeneo yasio halali, kutovunja nyumba hata moja bila kupata kibali kutoka kwa mkuu wa wilaya wa eneo husika.

Makonda aliyasema hayo jana wakati wa kumuapisha mkuu wa wilaya ya Ubungo, Kisale Makori aliyechukua nafasi iliyoachwa wazi na Humphrey Polepole ambaye aliteuliwa kuwa Katibu wa Kamati Kuu Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi, Itikadi na Uenezi.

“Kumekuwa na tabia ndani ya jiji hili ya kubomoa nyumba za wananchi masikini kwa kutumia nyaraka feki za mahakama. Mwisho wa siku watu wanabaki wanalia,” alisema Makonda

“Kwahiyo, ni marufuku kwa kampuni yoyote kuvunja nyumba bila kupata kibali cha mkuu wa Wilaya [wa eneo husika],” aliongeza na kusisitiza kuwa wakuu hao wa wilaya watafanya kazi ya kuhakiki nyaraka hizo ili kujiridhisha kama ni za mahakama.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa anahitaji kuanza mwaka mpya kwa amani hivyo hataki kuona watu wakilia.  

Video: Wafanyabiashara masoko ya Dar walia na msimu huu wa Sikukuu
Polisi waelezea jinsi walivyomhoji Lissu