Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amepiga marufuku watu kutoa pesa kwa ombaomba na watoto wanaoranda katika barabara za jiji hilo wakiomba pesa kwa wapita njia.

OMBAOMBA

Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa pamoja na kwamba wapita njia kuwapa pesa kunawafanya watu hao waendelee kuomba barabarani, wapo watu wanaowatumia watoto wadogo kuomba huku wao wakiwa wamekaa pembeni au majumbani, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.

Amesema watu hao wanaowatumia watoto kujipatia kipato kinyume cha sheria watachukuliwa hatua.

Katika kukabiliana na idadi inayoongezeka ya watoto wanaoomba mitaani na kwenye barabara za jiji hilo, amesema kuwa uongozi wa jiji hilo kwa kushirikiana na Ustawi wa Jamii na Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa wamepanga kuwakusanya na kuwaweka watoto hao katika vituo maalum.

Operesheni ya kuwaondoa ombaomba katikati ya jiji la Dar es Salaam na kuwarudisha makwao ombaomba hao iliwahi kufanywa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mzee Yusuph Makamba.  Lakini operesheni hiyo haikuweza kuwa mwarubaini wa kuwaondoa watu hao jijini humo, wengi waliopelekwa mikoani kwao walirudi kwa nauli zao.

Chanzo: Channel 10

Vincent Kompany Kuwakosa Paris Saint-Germain Kesho
Ratiba Ya Nusu Fainali Kombe La Shirikisho Kufahamika Kesho