Wakati kukiwa na mjadala kwenye vyombo vya habari baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kueleza mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuwa alikataa hongo ya shilingi milioni 5 ya wauza shisha, mkuu huyo wa mkoa amefunguka zaidi.

Makonda amewataka wale wanaosubiri kuona anatumbuliwa wafahamu kuwa yupo kwa makusudi ya Mungu kuwatumia wananchi na kwamba ametumwa na Yesu Kristo kwa ajili ya kunyoosha mambo.

“Waacha waseme, waandike wawezavyo lakini wajue kuwa mimi ni mwamba imara nimeletwa na Yesu ili kuokoa hiki kizazi,” Makonda alisema jana kwenye Power Breakfast ya Clouds Fm.

Mkuu huyo wa mkoa alionesha kuwashangaa baadhi ya waandishi wa habari ambao walijikita katika kuichambua kauli yake iliyotafsiriwa kama mashtaka kwa Waziri Mkuu dhidi ya Kamanda wa Polisi mkoa wa Dar es Salaam, Simon Sirro pamoja na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Robert Boaz kuwa huenda walipitiwa na hongo aliyoikataa ya wafanyabiashara wa Shisha.

“Jana ilikuwa siku ya mtoto njiti duniani, moja ya madhara ya shisha ni watoto kuzaliwa njiti. Kwanini wasiandike habari hizi wanajali kauli?” Makonda alihoji.

Mkuu huyo wa Mkoa wa Dar es Salaam alisisitiza kuwa hakuwataja hadharani majina ya wafanyabiashara waliotaka kumpa hongo kwa sababu tayari yalishapelekwa kwa vyombo husika [Takukuru].

Katika hatua nyingine, Makonda ameanzisha kampeni mpya aliyoipa jina la ‘Dar es Salaam Mpya’. Kupitia kampeni hiyo, atazunguka mkoa huo kusikiliza kero za wananchi na kuzifanyia kazi.

Ruge akimulika kipaji cha Ruby, aeleza anapomuona baada ya kuitosa THT
Maalim Seif, Mtatiro kufuta nyayo za Lipumba Kusini