Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda anaendelea na operesheni ya kulisafisha jiji la Dar es Salaam ambapo sasa ametangaza vita dhidi ya watu wanaojishughulisha na mapenzi ya jinsia moja (mashoga) na wasichana wanaofanya biashara ya ukahaba.

Makonda amesema kuwa Serikali haitavifumbia macho vitendo hivyo ambavyo ni kinyume cha maadili ya kitanzania na ambavyo vinaongeza maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi.

Amesema atahakikisha anawaondoa wale wote wanaojihusisha na vitendo hivyo na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Wiki iliyopita, wananchi mbalimbali pamoja na baadhi ya wabunge waliinyoshea kidole ‘Clouds Tv’ kwa kurusha kipindi cha ‘Take One’ kilichomhoji Shoga maarufu. Hata hivyo, Mkuu huyo wa Mkoa alikitetea kituo hicho cha runinga na kueleza kuwa kilichofanya ni kuonesha ukubwa wa tatizo lililopo katika jamii ili litafutiwe ufumbuzi.

Hii ni operesheni nyingine aliyoitangaza Makonda ikiwa ni miezi michache baada ya kutangaza kuwaondoa ombaomba wote katika mitaa ya jiji la Dar es Salaam.

Vita dhidi ya ombaomba na makahaba iliwahi kuendeshwa kwa kiwango kikubwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mzee Yusuf Makamba. Hata hivyo, hivi karibuni, Mzee Makamba aliiambia Clouds Fm kuwa aliweza kufanikiwa katika operesheni ya kuwaondoa ombaomba kwa kiasi kikubwa lakini alikiri kuwa ‘madada poa’ walimshinda kuwaondoa.

Mapema mwaka huu, Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro alitangaza operesheni ya kuwakamata wanaofanya biashara ya ukahaba pamoja na wateja wao, uamuzi ambao uliongezwa nguvu na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

 

Khloe Kardashian afichua siri ya maisha kati yake na The Game
Video: Taarifa kutoka TRA kuhusu 18% VAT kwenye huduma za fedha