Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema kuwa atahakikisha anawashughulikia kwa mujibu wa sheria na mamlaka aliyonayo, wanaume wanaokataa kuitikia wito wa kufika katika ofisi zake kujibu tuhuma za kutelekeza watoto na kupima vina saba (DNA).

Akizungumza kupitia TBC1, Makonda amesema kuwa wanaokataa wito huo wakidhani kuwa hadhi yao ni muhimu zaidi wanapaswa kufikiria tena kwani bahati nzuri watu hao  wanamfahamu hata kabla hajawa mkuu wa mkoa.

“Yoyote anayekaidi wito wa Ustawi wa Jamii ambao wako chini yangu, achilia mbali kwamba anakuwa amefanya kosa kwa mujibu wa sheria, kwa mamlaka tu niliyonayo mimi nakutia ndani,” alisema.

“Yaani na bahati mbaya niwaambie tu Watanzania, kwangu sheria ina nafasi kubwa sana kuliko hadhi unayojitengenezea ambayo kimsingi huna kama umeamua kutelekeza mtoto. Tusijaribiane,” aliongeza.

Mkuu huyo wa mkoa alieleza kuwa anayetunisha misuli ya kutoitikia wito anapaswa kufikiria kuwa kama anaweza kumuondoa mtu kwenye mkoa huo anapoona anahatarisha usalama na kuvunja amani, itakuwaje kwa hilo la mtu kumtelekeza mtoto.

Alisema kuwa awali, wanasiasa waliokuwa wanajinasibu kuwa hawahusiki na kinachoendelea na kwamba ni mpango wa kuchafuana kisiasa wameanza kuwa wapole baada ya kuona mama na watoto waliowatelekeza wakijitokeza na kuzungumza hadharani.

Akizungumzia hatua anazoweza kuwachukulia watu hao, Mkuu huyo wa mkoa amesema kuwa baada ya Ustawi wa Jamii na dawati la wanawake la Polisi kukamilisha kazi ya kuwaita wanaolalamikiwa kukamilika, watampa ripoti ya walioitikia wito na waliokataa pamoja na hatua walizofikia na ndipo waliokaidi watajua wigo wa mamlaka yake.

“Nikiambiwa haya mashauri yamebaki hayajashughulikiwa kwa sababu walioitwa wamegoma kuja… sasa hapo ndipo utaelewa Makonda ni Mkuu wa Mkoa, mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama au  ni mtoto wako unayeweza kumuendesha kama unavyoweza kuchezea sharubu za Simba aliyelala,” alisema.

Miongoni mwa watu maarufu wanaotakiwa kufika katika ofisi za mkuu huyo wa mkoa ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ambaye analalamikiwa na mwanamke mwenye umri wa miaka 31 kuwa ni mtoto wake aliyemtelekeza. Mama mzazi wa mtoto huyo pia alifika katika ofisi hizo na kueleza kuwa anachosema mwanaye ni kweli kwa mba baba yake ni mzee Lowassa.

Lowassa alipozungumza na gazeti la Mwananchi alieleza kuwa tuhuma hizo kwake sio za kweli na hazina msingi. Alipoulizwa kama ataenda kupima DNA kama inavyoelekezwa na mkuu wa mkoa, alisema, “kwangu kupima DNA [kuhusu hilo] ni upuuzi. Hizo ni siasa za kuchafuana.”

Mwingine aliyeguswa na sakata hilo ni mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa ambaye naye amekataa kufika ofisi za mkuu wa mkoa na kumtaka mwanamke anayedai kuwa alizaa naye na kumtekeleza afike katika ofisi za bunge ataonana naye.

Msigwa alisema kuwa endapo itathibitika kuwa ni mwanaye yuko tayari kuacha ubunge.

 

Serikali kuimarisha ulinzi baharini
Muigizaji aanguka na kufariki 'akishuti' filamu