Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda amepiga marufuku watu wasiooga au kufua nguo zao kuonekana mjini katika kipindi cha mwezi Agosti wakati wa mkutano wa wakuuu wa nchi za jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika (SADC) ambao unatarajiwa kuhudhuriwa na watu zaidi ya 1000.

Mkutano huo wa 39 wa SADC unatarajiwa kufanyika mwezi ujao, Agosti 17 na 18 na kuhudhuriwa na wakuu wa nchi 16 wanachama wa jumuiya hiyo.

Hayo ameyasema leo, Julai 29 wakati wa uzinduzi wa kampeni ya tano ya usafi yenye lengo la kuendeleza kufanya usafi katika jiji la Dar es salaam ikiwa ni hatua za mwanzo za maandalizi ya kupojea ugeni wa viongozi wa SADC.

“Tabia ya kuja mjini hujafua, hujaoga usitutie aibu kama umezoea kuja mjini hujaoga wala kufua nguo baki nyumbani walau huu mwezi wa nane uishe, tunataka sio usafi tu wa mazingira, usafi pia wa wananchi wetu, watu wamejaa chawa tu hapa”. Amesema.

Sababu ya kutoa amri hiyo kwa mujibu wa Makonda ni kuepuka “kumtia aibu Rais wa Tanzania John Magufuli mbele ya marais kutoka nchi 15 watakaokuwa hapa nchini.”

Hivyo Mkuu wa Mkoa amepiga marufuku mtu yeyote kufika mjini kama hajafanya usafi wa mwili wake ikiwemo kuoga na kupiga pasi nguo zake.

Aidha Makonda amehimiza suala la usafi na kuwaagiza wanajeshi na wanamigambo waliosambazwa kwa ajili ya kufanya usafi wa jiji, kuhakikisha wanamchukulia hatua dereva wa gari binafsi atakayetupa taka hovyo.

Shughuli za usafi katika jiji hilo kwaajili ya mkutano wa SADC zinatarajiwa kuanzia leo kuendeshwa na vijana 130 wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na mgambo 300 katika maeneo mbalimbali ya jiji.

 

Video: MacLeans BeneCIBO yawaneemesha wakulima kimasoko
Boko Haram wafanya shambulio mazishini, 65 wauawa vibaya