Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewaonya wanunuzi wa makontena yake yanayopigwa mnada kwenye Bandari ya Dar es Salaam kuwa wasifanye hivyo kwani watalaaniwa wao na uzao wao.

Makontena hayo 20 ambayo ndani yake kuna vifaa vya shule ikiwa ni pamoja vifaa vya ofisi za walimu yalishindwa kununuliwa kwenye mnada wa Jumamosi baada ya wanunuzi kushindwa kufika bei iliyotajwa. Mnada wa makontena hayo umeitishwa baada ya Makonda kushindwa kuyalipia kodi.

Makonda ameeleza kuwa atahakikisha makontena hayo hayanunuliki kwani amemuomba Mungu azuie uuzwaji wake.

“Nipo kanisani, kanisa la Angilikana huku Ngara mkoa wa Kagera. Nitafanya ibada maalum kuhakikisha makontena hayo hayauziki kamwe kwa mtu yeyote kwa sababu tuliyaingiza nchini kwa ajili ya Walimu maskini katika mkoa wetu,” Makonda anakaririwa na The Citizen.

Alifafanua kuwa makontena hayo yaliingizwa nchini kwa jitihada zake binafsi kwa lengo la kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli katika kuboresha elimu nchini.

Alisema kuwa hawezi kukaa kimya na kutofanya lolote wakati anaona dhahiri namna ambavyo Rais Magufuli anapenda na anaipa kipaumbele elimu.

Alitoa wito kwa mtu yeyote mwenye mapenzi mema kusaidia kusukuma zaidi gurudumu la maendeleo ya sekta ya elimu katika mkoa wake.

Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo alisema kuwa mmiliki wa makontena hayo alipewa siku 30 kuhakikisha analipia kodi, vinginevyo yatapigwa mnada. Makontena hayo 20 yalikuwa miongoni mwa makontena 80 yaliyokuwa yamenasa bandarini kwa kutolipiwa kodi.

Video: Goodluck Gosbert asimulia alivyopata mualiko Ikulu
Hatima ya Nondo kujulikana leo