Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda leo Julai 11, 2017 ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la kisasa la huduma za dharura Hospitali ya Temeke ambalo ujenzi wake utagharimu zaidi ya shilingi Million 800 na ujenzi huo unalofadhiliwa na ubalozi wa Japan Nchini Tanzania.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Makonda amesema jengo hilo litakuwa na uwezo wa kusaidia zaidi ya watu 2,000 kwa siku ambapo litakuwa na chumba cha upasuaji, chumba cha ICU, vyumba vya uangalizi maalumu wa wagonjwa pamoja na vyumba vya madaktari.

Aidha jengo hilo litakuwa na vyumba maalumu vya watoto (njiti) akinamama na wababa ambapo lengo ni kuhakikisha mgonjwa yoyote wa dharura iwe wa ajali,upasuaji kwa kinamama wajawaziito,malaria ya ghafla,moto na wanaobanwa na kifua wanapatiwa huduma ya haraka ambapo kwa hatua hiyo itasaidia kupunguza mlundikano wa wagonjwa wa dharura Hospital ya Taifa Muhimbili kama Rais Dkt.Magufuli anavyotaka.

“Mimi nimeshuhudia watu wengi wakipoteza maisha kwa kukosa huduma za dharura, hii ndio iliyonisukuma kutafuta kila njia ili wananchi wangu wasipoteze maisha kwasababu tu ya kukosa hutuma ya haraka, nikaamua kumtafuta balozi wa Japani na kumshirikisha jambao hili, Balozi aliponisikiliza na kunielewa akakubali kuniunga mkono katika mapambano yangu ya kuboresha huduma za afya kwa wananchi hasa wanyonge na ameshanipa  fedha kwaajili ya ujenzi wa jengo hilo na hivi tunavyoongea tayari mkandarasi ameanza na ujenzi” Amesema Makonda.

Aidh, Makonda amesema kuwa ujenzi wa jengo hilo utachukuwa miezi sita hadi kukamilika na kueleza kuwa dhamira yake ni kuhakikisha Dar es salaam inakuwa mkoa unaotoa huduma bora za Afya.

“Watu hatukumbukwi kwa maneno bali kazi tulizofanya, kwa kuwa Rais Magufuli amenipa Mkoa niongoze na mimi ni lazima nitumie akili na kipaji ambacho Mungu amenipa kutatua Changamoto za Afya katika Mkoa wangu”, Amesisitiza Makonda.

Kwa upande Mwakilishi wa Balozi wa Japani Nchini Tanzania Bwana Hiroyuki Kubota amesema serikali ya Japan itaendelea kushirikiana na Tanzania katika masuala mbalimbali huku mkuu wa wilaya ya Temeke Mheshimiwa Felix Lyaniva akimpongeza Makonda kwa namna anavyopambana kutatua kero za wananchi.

Magazeti ya Tanzania leo Julai 12, 2017
Mchezo Wa Kirafiki Kati Ya Gor Mahia Na Everton