Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametoa onyo kwa watu wanaompigia simu kumpa taarifa kuhusu uwepo wa rushwa makanisani wakitaka polisi wakawakamate.

Makonda alitoa onyo hilo jana alipohudhuria ibada ya Pasaka katika Kanisa la Agrikan la Mtakatifu Albano jijini Dar es Salaam baada ya kupewa nafasi na Askofu Mkuu wa Kanisa la hilo Tanzania, Askofu Valentino Mokiwa.

Alisema kuwa Kanisa ni Taasisi ambayo ina mfumo wake wa uongozi ambao unapaswa kushughulikia matatizo yote kwa kufuata ngazi na taratibu za kikanisa kwa njia ya kiroho kabla ya kukimbili Polisi ambao ni watu wa dunia.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa anashangazwa na kuwepo kwa ripoti za rushwa na vitendo viovu katika nyumba za ibada na kuwataka Maaskofu na Wachungaji kukemea na kushughulikia matatizo yao kabla ya kuwekwa hadharani kwa watu wa dunia kupitia mfumo wa serikali.

Alisema aliwahi kupokea simu kutoka kwa muumini mmoja aliyemtaka atume Polisi katika kanisa ambalo hakulitaja jina lakini alimpa onyo kuwa endapo atampigia simu kama hiyo tena atatuma polisi wamkamate yeye kwanza kwani alipaswa kutoa taarifa kwa viongozi wa dini hiyo kabla ya kukimbilia polisi.

“Nawaambia, mtu ukinipigia simu kunambia kuna watu wanatoa au kupokea rushwa kanisani. Kwanza ntakuweka ndani wewe,” alisema Makonda.

“Serikali inahitaji msaada wa kanisa na viongozi wa dini ili iweze kufanya kazi vizuri. Sitaki kusikia polisi wanakwenda kanisani [kukamata] katika mkoa wangu na wale wanaotoa taarifa kutaka polisi nitawaweka ndani,” aliongeza.

Kadhalika, Makonda alitumia muda huo kuwasisitiza wakazi wa Dar es Salaam kuhakiki silaha zao kwani Jeshi la Polisi litaendesha operesheni maalum baada ya kipindi husika kupita.

Awali, Askofu Mokiwa aliwataka waumini kuhakikisha kuwa hawakimbilii kuita vyombo vya habari pale ambapo kunatokea migogoro katika nyumba za Ibada bali wafuate mfumo wa kiroho wa kikanisa.

 

Vanessa Mdee azungumzia mpango wa kufunga ndoa
Mbunge Afunguka walivyoitiwa 'Rushwa' kwa lugha tamu