Aliyekuwa Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk. Makongoro Mahanga amekosoa uteuzi wa makatibu wakuu na manaibu katibu wakuu alioufanya hivi karibuni Raisi Magufuli akidai kuwa hauendani na dhamira yake ya kupunguza ukubwa wa serikali na kubana matumizi.

Kupitia ujumbe wake alioutuma kwenye mitandao ya kijamii, Mahanga alimkosoa rais Magufuli kwa kuwateua makatibu wakuu 27 ili hali ana waaminisha wananchi kuwa wizara ni 15 pekee.

“Sio kweli kwamba amepunguza ukubwa wa Serikali bali ameongeza ukubwa wake. Sina uhakika kama washauri wa rais wamemshauri na kumueleza kwamba wizara sio ofisi ya waziri bali wizara ni ofisi ya katibu mkuu,” alisema Dk. Mahanga.

Rais Magufuli aliteua Mawaziri 15 na manaibu waziri 19 hivyo kufanya baraza lake la mawaziri kuwa na jumla ya mawaziri 34, tofauti na jumla ya mawaziri 55 wa serikali ya awamu ya nne.

Hata hivyo, Dk. Mahanga alimsifia rais Magufuli kwa kazi aliyoifanya ya kupambana na wala rushwa na wakwepa kodi.

“Kweli alitumbua majipu ambayo yalikuwa yameiva. Naweza kusema alikuta nyumba chafu na inanuka, ameisafisha. Sasa tunapenda kuona baada ya kuisafisha ataiweka katika hali gani? Atabuni nini ili kuwasaidia vijana katika suala la ajira ili wengi waweze kumudu gharama za maisha,” Mahanga alimwambia mwandishi wa gazeti la Mwananchi.

Sikuelewi! Utajiri Huu wa Ridhiwani Ni wa Kutisha
Serikali Yazidi Kuwabana Watumishi Watakaofanya Makosa