Kenya maafisa wa polisi mjini Eldoret wamewatia mbaroni makurutu 99 baada ya kufika katika kambi ya mafunzo ya Moi Barracks wakiwa na barua feki za kujiunga na jeshi .

Makurutu hao walikamatwa ili kuwezesha maafisa wa polisi kufanya uchunguzi kubaini walikozitoa barua hizo.

Akizungumza na wanahabari mjini Eldoret, Msemaji wa KDF, Kanali Paul Njuguna alisema baadhi ya makurutu walikiri kutumia hongo ili kujiunga na jeshi.

“Nashangaa vijana hao walizitoa wapi barua hizi, shughuli ya kuwachagua makurutu ilifanyika katika vituo ambavyo vilichapishwa rasmi kwenye magazeti na hata kutangazwa katika vyombo vya habari,” Njuguna alisema.

Njuguna alisisitiza kuwa shughuli yoyote iliyofanywa nje ya vituo hivyo haikuwa halali.

Baadhi ya makurutu walisimulia jinsi walivyouza ardhi zao ili kupata fedha za kulipa hongo kabla ya kukabidhiwa barua hizo feki.

Kwa sasa Kanali Njuguna amewaonya Wakenya kujitahadhari na watu wanaotumia ukosefu wa kazi miongoni mwa vijana kuwahadaa na kuwafilisi fedha zao.

Mvua kali zaua watu 46 wengine 28 haijafahamika walipo Brazil
Sentensi 5 za Bryant zitakazoishi milele masikioni mwa watu

Comments

comments