Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Dodoma imepokea malalamiko nane yenye viashiria vya rushwa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajia kufanyika Novemba 24, 2019 nchini.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Dodoma Sosthenes Kibwengo amesema taarifa hizo zimewasilishwa na wananchi wa kata mbalimbali za wilaya zilizopo mkoani hapa zikihusisha masuala ya chaguzi.

“Taarifa hizi zimewasilishwa na wakazi wa maeneo tofauti toka wilaya mbalimbali baada ya kubaini baadhi ya wagombea watarajiwa wanashinikiza majina yao yapitishwe kwa ajili ya kuwania kuchaguliwa katika nafasi mbalimbali za uongozi,” amebainisha Kibwengo.

Amesema mara baada ya kupokea taarifa hizo TAKUKURU imeanza kuzifanyia kazi ili kuweza kujiridhisha kama malalamiko hayo yana ukweli ndani yake na endapo itathibitishwa basi sheria itachukua mkondo wake kwa wahusika ili waweze kufikishwa Mahakamani.

Aidha katika hatua nyingine Kibwengo amewatahadharisha wananchi na viongozi wa ngazi mbalimbali katika Mkoa wa Dodoma kuwa makini na vitendo vya utapeli vilivyoibuka vya kutumia jina lake kutapeli watu.

Amesema kumekuwa na vitendo vya utapeli ambavyo vimeibuka kwa baadhi ya watu wasiofahamika kutumia majina ya viongozi mbalimbali kwa kutuma ujumbe wa simu na au kuwapigia wakiomba fedha kwa madai ya kuwasaidia mambo yasiyo sawa kwenye ofisi zao.

“Wananchi na viongozi wawe makini mana kuna watu wanatuma sms wakidai ni wakuu wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma na katika ofisi za umma wakida kuna mambo hayako sawa hivyo watoe fedha kurekebisha mambo hayo” amefafanua Mkuu huyo.

Kimbwengo amebainisha kuwa tangu mwezi machi hadi Oktoba 2019 wamepokea malalamiko manne ya watu kutoka maeneo mbalimbali wakidai kupigiwa simu na mkuu wa TAKUKURU kuwa watoe fedha ili kurekebisha hali ya sintofahamu iliyopo katika ofisi zao.

Ameongeza kuwa TAKUKURU inafanya kazi kwa kufuata taratibu na sheria ya majukumu yake ya kila siku na kwamba kama kuna tatizo mtu anahojiwa ofisini na sio kupigiwa simu na endapo kuna malipo yeyote hufanywa kwa mfumo husika uliowekwa kwa mujibu wa sheria.

Mlevi aliyemtishia polisi paka atupwa jela miaka 5
Mo Dewji asimulia Maombi yalivyo mchomoa kwa Watekaji