Wakati mikutano ya kampeni za wagombea urais kupitia Chadema na CCM ikionekana kuhudhuriwa na mafuriko ya wananchi ukilinganisha na wagombea wengine hali inayowafanya waonekane kuwa na nguvu kubwa wakiwaancha wengine kwa mbali, mgombea urais kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, Bi. Anna Mghwira amerusha ‘jiwe’ kwa waandaaji wa mikutano ya wagombea hao.

Akiongea katika mahojiano maalum na BBC mapema leo asubuhi, Bi. Anna Mghwira ambaye anaonekana kuwa na nguvu katika uwanja wa siasa akiwa mwanamke pekee anayegombea nafasi hiyo ya juu zaidi serikalini, alisema kuwa mikutano ya wagombea hao inajazwa kwa mtindo wa kuwabeba watu kwenye magari, jambo ambalo chama chake hakitaweza kufanya daima.

“Vyama hivyo vinapesa kwa hiyo vinabeba watu kwenye magari vinawapeleka kwenye majukwaa wanajaa. Sisi hatuna hizo pesa za kuwabeba, na hata kama tungekuwa nazo tumeshasema hatutawabeba wananchi kuja kwenye mikutano yetu,” alisema Bi. Mghwira.

Katika hatua nyingine, Bi. Mgwhira alisema kuwa anaunga mkono sera za wagombea wenzake kuhusu suala la elimu bure na kwamba amejipanga kuboresha elimu kwa kiwango kikubwa zaidi endapo atachaguliwa kuwa rais wa Tanzania.

Jina la Bi. Anna Mghwira limefahamika kwa watanzania wengi katika kipindi hiki cha uchaguzi lakini licha ya kutokuwa kwenye siasa kwa muda mrefu, uwezo wake wa kujieleza na sera za chama chake zimekuwa kivutio cha wananchi wengi wanaomuunga mkono katika uchaguzi huu. Wataalam wa masuala ya siasa wanampa nafasi ya tatu kama mgombea mwenye nguvu zaidi kati ya wagombea urais wanane wanaoshindana.

 

Kamati Ya Taifa Stars Yatambulishwa Rasmi
CCM Kuzuia Wanafunzi Wa Vyuo Wanaosafirishwa Kupiga Kura