Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kuendelea kuuenzi mwenge wa uhuru na mbio za mwenge kwani falsafa yake inahitajika zaidi sasa kuliko wakati mwingine.

Akiongea jana wakati wa uzinduzi wa mbio za Mwenge uliofanyika katika Uwanja wa wa Jamhuri Mkoani Morogoro, Mama Samia alisema kuwa mwenge wa Uhuru umekuwa kichocheo cha maendeleo nchini pamoja na kuhamasisha amani, upendo, heshima na mshikamano tangu ulipowashwa mwaka 1964.

Alisema kuwa wakati huu mwenge huo unahitajika zaidi kwani kuna hali ya kudharauliana na kuanza kujengeka kwa hali ya kukatishana tamaa na chuki katika taifa.

Mwenge wa uhuru umekuwa ukizunguka katika maeneo mbalimbali nchini na kuzindua miradi mbalimbali ukiwa umebeba jumbe za kuimarisha umoja, amani, heshima, matumaini na upendo.

Katika hatua nyingine, mmoja kati ya viongozi wa Chama Cha Wananchi (CUF), Joseph Mtatiro amekosoa uwepo wa mbio za mwenge katika serikali ambayo imekuja na mkakati wa kubana matumizi na kwamba hilo ni jipu linalohitaji kutumbuliwa mapema.

Akiongea na Azam TV, Mtatiro alidai kuwa pesa nyingi zinatumika katika zoezi la kukimbiza mwenge lakini miradi inayozinduliwa mingi huishia kuwa imedumaa na huchukua miaka kadhaa kutekelezeka.

Alisema kuwa mwenge unatumiwa na chama tawala katika kueneza chama na kufanya utafiti wa namna wanavyokubalika nchini.

Serikali yaweka wazi Muda wa kutua nchini ndege mpya za Magufuli
Magufuli amtumbua jipu Mkurugenzi wa Jiji Dar, Makonda amshtaki