Mtu mmoja amefariki na wengine wanne akiwemo mke wa Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Peter Pinda, Mama Tunu Pinda wamejeruhiwa katika ajali mbaya ya gari iliyomhusisha mwendesha pikipiki katika Manispaa ya Morogoro.

Ajali hiyo imetokea Februari 8, majira ya saa nane mchana katika eneo la Mkundi, barabara ya Morogoro – Dodoma katika manispaa hiyo, baada ya gari lililombeba Mama Pinda aliyekuwa akisafiri kutoka kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam lilimgonga mwendesha pikipiki huyo aliyekuwa akikatiza barabara.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Rajabu Rutengwe amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kuwataja wengine waliojeruhiwa ambao waliokuwa kwenye gari hilo lenye nambari za usajili STK 9242, kuwa ni dereva wa gari hilo Anjelo Mwisa, mlinzi wa mke wa waziri mkuu mstaafu, Gaudensi Tembo na kijana wa familia ya Mama Tunu Pinda ,Gilbert Sampa.

Akielezea hali ya Majeruhi, mganga mfawidhi wa hospitali ya mkoa wa Morogoro, Dk. Rita Liamuya alisema kuwa wanaendelea vizuri na kwamba wanatarajiwa kuhamishiwa jijini Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu zaidi.

Chanzo: ITV

Chui avamia shule katika jiji alilodhalilishwa mwanafunzi mtanzania nchini India
Magufuli aipa mahakama Mabilioni, serikali yasema zitasaidia hukumu ya wakwepa kodi