Mama wa muanzilishi wa kundi la kigaidi la Al-Qaeda amezungumza kwa mara ya kwanza kwenye mahojiano maalumu kuhusu mwanaye, ikiwa ni miaka saba tangu alipouawa.

Alia Ghanem amezungumza na gazeti la Uingereza la Gurdian akiwa mjini Jeddhah, Saudi Arabia ambapo ndipo Osama alipozaliwa na kukulia, kabla hajageuka kuwa mpiganaji na baadaye kiongozi wa kundi kubwa la kigaidi.

Mama huyo ameeleza kuwa familia yao kwa ujumla ilimuona Osama kwa mara ya mwisho mwaka 1999 ikiwa ni miaka miwili kabla ya shambulio la kigaidi la Septemba 9 nchini Marekani, alipokuwa Afghanistan.

Ameeleza kuwa wakati huo mwanaye alikuwa tayari ameshatajwa kuwa ni gaidi anayetafutwa zaidi duniani na Marekani, akiwa Afghanistan alipoenda kupambana dhidi ya vikosi vya wavamizi vya Kisoviet katika miaka ya 1980.

“Tulishtushwa kupita kiasi. Sikutaka haya yote yatokee. Kwanini aliamua kujitosa kiasi hiki,” Mama Ghanem alijibu swali la mwandishi aliyetaka kujua alivyojisikia baada ya kugundua mwanaye ni gaidi.

Mama huyo amesema kuwa enzi za utoto wake, Osama alikuwa mtiifu, mwenye sura ya aibu na mpole, lakini alibadilishwa akili na itikadi alipofika chuoni.

Wakati wa mahojiano hayo, kaka zake wawili ambao ni Hassan na Ahmad walikuwepo na walimueleza mwandishi wa habari kuwa walishtushwa na hatua aliyoichukua Osama na hasa waliposikia kuwa alihusika na ugaidi wa 9/11.

“Tangu tukiwa vijana hadi sasa, wote tuliona ametuaibisha. Tulijua sisi sote tutapa shida. Familia yetu wote walioko nje ya nchi walirejea Saudi,” alisema Ahmad.

Osama alikimbilia Pakistani mwaka 2001 baada ya kutekeleza shambulio la kigaidi nchini Marekani lililoua watu 3000. Alitoroka wakati ambapo Marekani ilianzisha mashambulizi makali nchini Afghanistan ikilenga kumuua.

Mwaka 2011, kikosi maalum cha makomando wa Marekani kilivamia makazi ya maficho ya Osama katika mji wa Abbottabad nchini Pakistani na kumuua. Watu wengine wanne waliouawa katika tukio hilo.

Kwa mujibu wa Marekani, mwili wa Osama ulizikwa baharini baada ya kufuata taratibu zote za mazishi ya imani ya Kiislamu kwenye ndege.

Wanaofua kondom na kutumia tena 'wafundwa'
Video: Ridhiwani azungumzia uchaguzi 2020, awashauri wapinzani