Imeelezwa kuwa Mshambuliaji Dejan Georgijevic ameamua kuvunja mkataba wake Simba SC, kufuatia kushindwa kutimiziwa mambo makuu matatu ambayo yaliainishwa kwenye mkataba wake klabuni hapo.

Mshambuliaji huyo juzi Jumatano (Septemba 28) aliamua kuondoka kambini Zanzibar, baada ya kutoa taarifa ya kuvunja mkataba wake katika mtandao wa Instagram.

Jambo la kwanza ambalo linatajwa kuwa sababu kubwa kumuondoa Dejan Simba SC ni kwamba tangu alipofika nchini Agosti 7, alikuwa akiishi katika moja ya hoteli kubwa iliyopo Mbezi baada ya kushindwa kupata nyumba ya kuishi iliyokuwa na vigezo vyake kwani kila alipokuwa akienda kukagua alipakataa.

Jambo la Pili ni kutokana na kushindwa kupatiwa baadhi ya stahiki zake walizokubaliana na uongozi wa Simba kwa wakati tangu anasaini mkataba wa kuitumikia timu hiyo.

Miongoni mwa maslahi hayo ni mshahara wake, bonasi pamoja na pesa ya usajili.

Jambo la Tatu ni kutoridhishwa na hali ya mambo kwa ujumla ndani na nje ya uwanja yalivyokuwa yanaendelea ndani ya timu hiyo.

Hata hivyo Uongozi wa Simba SC umetoa taarifa za kumchukulia hatua za kisheria Mshambuliaji huyo kwa madai amevunja mkataba kwa kushindwa kufuata taratibu zinazotambulika kisheria.

Rais Samia ahofia vijana kukosa nguvu za kiume
Magari yagongana na kuwaka moto, kuna vifo na majeruhi