Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amethibitisha tukio la kuibwa kwa kompyuta za Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) zilizokuwa na nyaraka za kesi za uhujumu uchumi.

Kamanda Mambosasa ameeleza kuwa jeshi hilo lilipokea taarifa hizo Jumanne, Oktoba 15, 2019 na linaendelea na uchunguzi.

“Ni kweli tukio hilo limetokea na polisi tumepokea taarifa Jumanne asubuhi, mpaka sasa hakuna mtu anayeshikiliwa kuhusiana na tukio hilo,” Kamanda Mambosasa anakaririwa na Gazeti la Nipashe.

Hata hivyo, hakueleza idadi ya kompyuta zilizoibwa. DPP alipotafutwa hakuweza kuzungumza akieleza kuwa yuko kwenye kikao.

DPP amekuwa katika mchakato wa kupokea barua za watu wanaokiri kuhujumu uchumi ambao wamemuandikia wakiahidi kurejesha fedha hizo kutokana na maagizo ya Rais John Pombe Magufuli.

Moja kati ya kesi maarufu ya uhujumu uchumi iliyoko mikononi mwa DPP ni ile ya IPTL inayowahusu Harbinder Sethi na James Rugemarila, wanaodaiwa kutakatisha zaidi ya Sh 309 bilioni.

Video: Kompyuta za DPP zaibiwa, Magufuli aacha patashika Lindi
Video: Kijana aliyekuwa anapumulia mashine afariki dunia