Mahasimu wa soka katika mji wa Manchester, nchini England, Manchester City na Manchester United wametangaza kuweka kambi nchini Marekani kwa ajili ya kujiandaa na msimu 2018/19.

Kikosi cha Pep Guardiola kilichotawazwa kuwa mabingwa wa 2017/18 mwishoni mwa juma ililopita baada ya Manchester United kufungwa na West Brom bao moja kwa sifuri, kitafanya ziara ya kujiandaa na msimu mpya nchini Marekani mwezi Julai.

City wataanza maandalizi ya kujiandaa na msimu mpya kwa kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Borussia Dortmund katika uwanja wa Chicago’s Soldier Julai 20.

Baadae kikosi cha mabingwa hao wa England kitasafiri hadi mjini New Jersey kucheza mchezo wa pili wa kirafiki dhidi ya Liverpool Julai 25 katika uwanja wa MetLife Stadium.

Mchezo huo unatarajiwa kuwa na vuta ni kuvute, kufuatia wawili hao kuwa na upinzani mkali, hasa baada ya Liverpool kuiondosha Manchester City kwenye hatua ya robo fainali ligi ya mabingwa barani Ulaya.

Baada ya mpambano dhidi ya majogoo wa jiji, Manchester City watamaliza ziara yao ya siku tatu mjini Miami katika uwanja wa Hard Rock kwa kupambana na waajiri wa zamani wa meneja wao pep  Guardiola FC Bayern Munich.

Kwa upande wa kikosi cha Jose Mourinho (Manchester United), kitacheza dhidi ya Liverpool, Real Madrid na kisha AC Milan katika michuano ya ICC.

Michezo mingine ya maandalizi ya Manchester United itakua dhidi ya Club America (Julai 19) mjini Glendale – Arizona, San Jose Earthquakes (Julai 22) mjini Santa Clara-California, kabla ya kuanza kushiriki michuano ya ICC.

Mchezo kati ya Manchester United dhidi ya AC Milan utachezwa Julai 25 kabla ya kuwakabili Liverpool Julai 28, na Julai 31 watacheza dhidi ya Real Madrid.

Mchezo dhidi ya Liverpool utachezwa kwenye uwanja wa “The Big House” mjini Michigan, uwanja ambao uliweka rekodi ya dunia kwa kuchukua mashabiki 109,318, pindi mashetani hao wekundu walipocheza dhidi ya  Real Madrid mwaka 2014.

Burundi yatuhumiwa kwa kuminya uhuru wa wapinzani
Chelsea hatarini kumkosa Marcos Alonso nusu fainali kombe la FA

Comments

comments