Uongozi wa klabu ya Manchester United umefikia makubaliano na klabu ya Ajax Amsterdam iliyowasilisha ombi la kumrejesha kundini beki/kiungo kutoka nchini Uholanzi Daley Blind.

Blind mwenye umri wa miaka 28 alijiunga na Man Utd miaka minne iliyopita akitokea Ajax Amsterdam, lakini changamoto ya kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza chini ya meneja Jose Mourinho, iliwavutia viongozi wa klabu hiyo ya Uholanzi kutuma ombi la kumrejesha kundini.

Kutumika kwa Ashley Young katika nafasi ya ulinzi, kumekua sababu kubwa ya Blind kushindwa kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara, katika mfumo wa Morinho.

Vyombo vya habari vya England vimeripoti kuwa, Blind atarejea Ajax Amsterdam juma hili, na ada yake ya uhamisho inatajwa kuwa Pauni milioni 14.1 sawa na Euro milioni 18.66.

Blind alijiunga na Man utd kwa ada ya Pauni milioni 14, baada ya kuonyesha kiwango cha hali ya juu wakati wa fainali za kombe la dunia za mwaka 2014, na alipelekwa klabuni hapo na aliyekua meneja kwa wakati huo Louis Van Gaal, ambaye kabla ya hapo alikua kocha mkuu wa timu ya taifa ya Uholanzi.

Blind ataondoka Man Utd huku akiacha kumbukumbu ya kucheza michezo 54, kutwaa taji moja la kombe la FA mwaka 2016, ubingwa wa Europa league pamoja na kombe la ligi nchini England 2017.

Wastaafu kabla ya 1999 kuanza kulipwa
Video: Rais Magufuli afungua Mkutano wa Dunia wa Vyama vya Siasa