Hatimae uongozi wa Man Utd, umetangaza kumtimua meneja kutoka nchini Uholanzi Louis Van Gaal, ikiwa ni siku mbili baada ya kufanikiwa kutwaa ubingwa wa kombe la FA kwa kuifunga Crystal Palace mabao mawili kwa moja.

Maamuzi ya kutimuliwa kwa Van Gaal, yamefikiwa kutokana na makubaliano yaliyokuwepo hapo awali ya kuhakikisha anaiwezesha Man Utd inashiriki ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu wa 2016-17.

Van Gaal anaondoka Old Trafford, baada ya kukaa klabuni hapo kwa muda wa miaka miwili ambayo ni sehemu ya mkataba wake uliokua unatarajiwa kufikia kikomo mwishoni mwa msimu ujao.

Hata hivyo tetesi za kuondoka kwa mdachi huyo, zilianza kuchukua nafasi tangu mwishoni mwa juma lililopita na wakati mwingine vyombo vya habari vya England, viliripoti kwamba huenda angesalia klabuni hapo na kupewa nafasi ya ukurugenzi wa soka.

Hatua ya kuondoka kwa Van Gaal, inaendelea kutoa nafasi kwa aliyekua meneja wa klabu ya Chelsea, Jose Mourinho kuchukua nafasi ya ukuu wa benchi la ufundi la Man Utd, japo bado uongozi wa mashetani wekundu umeendelea kulikalia kimya suala hilo.

Kwa zaidi ya miezi minne sasa, Mourinho amekua akitajwa kama mbadala wa Van Gaal, na mashabiki wengi wanaamini huenda ujio wake huenda ukaleta mabadiliko ya kuondokana na kadhia ya kutofanya vizuri na kuwarejesha katika furaha kama ilivyokua wakati wa utawala wa Sir Alex Ferguson.

Waamuzi 40 Kuchezesha Ligi Ya Mabingwa Wa Mikoa
Video: Hospitali ya Mkoa wa Mwanza Sekouture kuanza kutoa huduma kwa watoto njiti