Nahodha na Mshambuliaji wa Timu ya Taifa ya Ureno Cristiano Ronaldo ana nafasi kubwa ya kuachana na Klabu ya Manchester United, wakati wowote kuanzia sasa.

Maamuzi ya Mshambuliaji huyo kuwa mbioni kuachana na Klabu hiyo wa mjini Manchester, yanakuja kufuatia sintofahamu iliyoibuka baada ya kufanyiwa mahojiano maalum, ambayo aliyatumia kuibua mzozo uliopo kati yake Meneja wa Manchester United, Erik ten Hag.

Uongozi wa Manchester United, umekiri kuchukizwa na alichokifanya Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 37, huku wadau wengine wakimtuhumu Ronaldo kwa kumwita ‘Mkosa Adabu’.

Hata hivyo pande hizo mbili zimeonyesha kuwa tayari kuachana kwa makubaliano maalum, ili kuondoa mzozo mkubwa ambao huenda ukajitokeza, endapo Ronaldo ataendelea kubaki klabuni hapo.

Hata hivyo taarifa iliyotolewa na Uongozi wa Manchester United, imeshindwa kutoa ufafanuzi wa kina ni lini pande hizo mbili zitakaa na kukubalina kuvunja Mkataba.

“Klabu inamshukuru kwa mazuri yote aliyoyafanya akiwa hapa Old Trafford,”

“Tunamtakia kila la kheri katika mipango na mikakati ya maisha yake mapya, kwa sasa kila mmoja klabuni hapa anaendelea na majukumu ya kuipeleka mbele Manchester United, chini ya Meneja Erik ten Hag.” Imeeleza taarifa iliyotolewa na Manchester United.

Manchester United kwa sasa ipo nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu ya England, ikiongozwa kwa mara ya kwanza na Meneja Ten Hag, ambaye alikabidhiwa jukumu hilo, mwanzoni mwa msimu huu 2022/23.

Kwa sasa Ronaldo yupo nchini QATAR akiwa na kikosi cha Ureno ambacho kinajiandaa na mchezo wake wa kwanza wa Kundi H dhidi ya Ghana utakaopigwa kesho Alhamis (Novemba 24).

Jumatatu (Novemba 21) Mshambuliaji huyo alizungumza na baadhi ya Vyombo vya Habari nchini QATAR na kusema: “Nitazungumza pale nitakapokua tayari kuzungumza, kwa sasa naangalia uwezekano wa kuisaidia Ureno kwenye Fainali za Kombe la Dunia.”

Ronaldo, tayari ameshaifungia Manchester United mabao 145 katika michezo 346 aliyocheza kwa vipindi viwili tofauti.

Hata hivyo amesaliwa na mkataba wa miezi saba katika kikosi cha Manchester United, huku akilipwa Mshara wa Pauni 500,000 kwa juma, na mpango uliopo ataondoka klabuni hapo kama mchezaji huru wakati wa Dirisha Dogo la Usajili Januari 2023.

Manchester United kuwekwa SOKONI
OHCHR yaikatalia Serikali hukumu ya kifo