Kamati ya Maadili ya Uchaguzi Ngazi ya Taifa, imekitaka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kiendelee kutekeleza maamuzi ya Kamati ya Maadili ngazi ya Jimbo la Ukonga yaliyokitaka chama hicho kusahihisha makosa yaliyotendeka na kuomba msamaha hadharani kwa kosa la kimaadili walilotenda.

Uamuzi huo umetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Jaji Mst. Mary Longway baada ya kikao cha kamati hiyo kupitia na kujadili rufaa dhidi ya uamuzi wa Kamati ya Maadili Jimbo la Uchaguzi Ukonga, iliyowasilishwa na Chadema Septemba 5, 2018 ikiitaka kamati hiyo itengue uamuzi wa Kamati ya Maadili ya Jimbo.

“Rufaa iliyowasilishwa yenye Kumb. Na. CDM/ILALA/MAADILI/2018/28 ya tarehe 5 Septemba, 2018 iliyopokelewa Tume tarehe 7 Septemba. Imewasilishwa nje ya muda wa saa 48 kinyume na maelekezo ya  kipengele cha 5.7 (b) cha Maadili tajwa. Hivyo, Kamati inaelekeza kuwa mrufani aendelee kutekeleza maamuzi ya Kamati ya Maadili ngazi ya Jimbo.”, amesema Jaji Mst. Longway.

Kwa mujibu wa uamuzi wa Kamati ya Maadili ngazi ya Jimbo la Ukonga, Chadema kimeonywa kuhakikisha kuwa kinafuata Kanuni na Taratibu za Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015 na kutekeleza maamuzi hayo ndani ya saa 48 tangu kutolewa na adhabu hiyo.

Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Ukonga, Jumanne Shauri mnamo Agosti 27, 2018 alipokea malalamiko na kupitia utetezi wa Chadema na kujiridhisha kuwa Chadema kilitumia kiongozi wa dini kumpigia kampeni mgombea wa chama hicho kinyume na kifungu cha 2.2 (k) cha Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015.

Msimamizi huyo wa Uchaguzi aliongeza kuwa “Dr. Makongoro Mahanga akiwa kiongozi wa Chadema, siku ya kampeni tarehe 25/8/2018 alitumia lugha ya matusi, kashfa, kejeli na udhalilishaji dhidi ya mgombea wa CCM, ikiwa pia ni kinyume na kifungu cha 2.2 (k) cha Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015″

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Septemba 12, 2018
Video: Rais mwenye mshahara mdogo aliyejipunguzia nusu ya mshahara wake