Mtoto wa Marehemu Alphonce Mawazo aliyetajwa kwa jina la Precious alikuwa mmoja kati ya waombolezaji waliotoa ujumbe wakati wa kuaga mwili wa baba yake katika viwanja vya Furahisha jijini Mwanza.

Mtoto huyo mwenye umri wa miaka 9 aliwatoa machozi waombolezaji baada ya kutoa ujumbe mzito wa majonzi huku akieleza kuwa atafuata nyayo za baba yake kuwa mwanasiasa mkubwa.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alieleza kuwa tayari kuna watu watatu ambao wameshajitokeza wakijitolea kumsomesha mtoto huyo wa Mawazo ikiwa ni pamoja na Edward Lowassa.

Pia, Mbowe alisema kuwa tayari wameshaongea na wabunge 113 wa Ukawa ambao wamejitolea kutoa kiasi cha shilingi 300,000 kila mmoja hivyo itapatikana shilingi milioni 33.9 ambayo itawekwa kwenye mfuko maalum wa kusaidia familia ya marehemu Mawazo aliyeuawa kikatili kwa kukatwa na panga mkoani Geita. Mawazo alikuwa Mwenyekiti wa Chadema, Mkoa wa Geita.

Huu ni ujumbe wa mtoto wa Marehemu Mawazo:

“Naitwa Precious Alphonce Mawazo. Nina vitu vinne tu vya kuwaambia. Kwanza namshukuru Mungu kwa yote, naamini ni mapenzi yake japo kwa kulazimishwa. Pili nashukuru uongozi mzima wa Chadema, makamanda na babu zangu Lowassa, Sumaye na mchungaji Mgiku (baba yake Mawazo).

“Umri wangu ni miaka 9 tu na mdogo wangu miaka miwili. Nimepata pigo kubwa, inauma sana. Nalaani mauaji ya kikatili na kinyama aliyofanyiwa baba yangu Alphonce Mawazo na kutuacha wadogo nikiwa mwanasiasa mkubwa… naomba mtuombee, mtusaidie na kutuongoza katika maisha yetu. Naiomba serikali na Tanzania nzima tuungane kukomesha mauaji ya kikatili.

“Damu ya baba yangu iliyomwagika itasimama juu ya kila aliyeshiriki kupanga na kutekeleza mauaji haya ya kinyama. Damu hii imemwagika kwa ajili ya haki na kumkomboa mtanzania.

“Na kipengele cha nne na cha mwisho, nawashukuru tena uongozi wa Chadema, ndugu jamaa na marafiki na watanzania wote mlioshiriki katika msiba huu mzito wa baba yetu. Asanteni sana!

 

Walimu Wacharuka Kudai Stahiki Zao Sengerema
Wamiliki wa Maduka Ya Dawa Baridi Walia Na Kasi Ya Magufuli