Madiwani wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wametakiwa kuitisha vikao vya Halmashauri Kuu katika Kata zao ili kujadili tathmini za utekelezaji wa ahadi mbalimbali zilizotolewa na Viongozi Wakuu wa Kitaifa wakati kampeni za uchaguzi mkuu ili kuondoa chuki kwa Serikali yao.

Agizo hilo limetolewa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania bara, Philip Mangula wakati wa Kikao cha tathimini cha kazi cha Chama cha Mapinduzi wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe, ambapo amesema jambo hilo likifanyika itawasaidia wananchi kujua miradi inayotekekezwa na Serikali kwa Kipindi husika.

“Madiwani muitishe vikao vya Halmashauri Kuu na mkawaeleze wananchi vitu vinavyotekelezwa vinavyoonekana kama miradi mbalimbali inayotekelezwa katika Kata zenu na kisiwe kitu cha kufikirika hiyo itaondoa chuki kwa wapiga kura’’ amesema Mangula.

Mbunge ni wajibu wake sasa, isitokee mtu mwingine akatoa misaada huyo ni mbabaishaji na ni mgogoro….Mbunge ni wakati wako sasa kuwajibika kwa wananchi” amesema Mangula.

Mangula amesema kwa kuwa CCM inaingia kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu, utaratibu wa madiwani hao kwenda kwa wananchi kutawafanya waelewe nini kinachoendelea kwenye Kata zao.

“Nawapongeza sana mkuu wa wilaya, Mbunge kwa kuwakutanisha viongozi wa Kata na Shina wa CCM, kuungana na mimi kusikiliza yaliyotekelezwa katika mwaka mmoja, tumeona mafanikio mengi mnayojivunia kama vile afya na maji kwa kuyatangaza kwenye serikali ya kijiji, hayo ndiyo maandalizi ya uchaguzi wa serikali ya mitaa,” amesema Mangula.

Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Wanging’ombe, Gerson  Lwenge alimweleza Mangula kwamba katika jimbo lake kuna changamoto kubwa ya maji na  hivyo alimshauri Rais na kumkumbusha juu ya suala la maji, ambapo alisema Rais Magufuli tayari ameidhinisha  shilingi zaidi ya bilioni 80 za kutatua kero za maji wilayani Wanging’ombe.

“Malengo ya taifa kwa Watanzania ni kupata maji asilimia 85 katika umbali wa mita 400, lakini sisi Wana Wanging’ombe tupo chini katika hizo asilimia,” amesema Lwenge.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Njombe, Jasery Mwamwala amemweleza Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Mangula kwamba kumekuwepo na ucheleweshaji wa malipo ya utekelezaji wa miradi ya maji kwa wakandarasi na kuiomba Wizara ya Maji ilitazame suala hilo kwa kuwa miradi mingi haiendi.

Katika kikao hicho Mangula alikabidhi pikipiki mbili kwa Jumuiya ya Vijana ya Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) zilizotolewa na Mbunge Lwenge kwa ajili ya kuanzisha mradi wa kuimarisha jumuiya hiyo kimapato.

Video: Lissu amaliza matibabu, aandaa waraka mzito
Bashir Ngangari agoma kuachia Urais