Mwenyekiti wa Klabu ya Simba SC Murtaza Mangungu amepangua hoja za baadhi ya Wachambuzi wa Soka la Bongo kuhusu ujio wa Kocha Mkuu mpya wa klabu hiyo Zoran Manojlovic, katika kipindi hiki ambacho tayari Uongozi umeshafanya sehemu ya usajili wa wachezaji.

Kocha Zoran Manojlovic alitangazwa kuwa Kocha Mkuu Simba SC Jumanne (Juni 28), siku moja kabla ya msimu wa 2021/22 kufikia kikomo, huku Simba SC ikitangaza kuachana na Rally Bwalya na Pascal Serge Wawa.

Mangungu amepangua hoja za Wachambuzi kuhusu kocha huyo kutoka nchini Serbia, baada ya kuulizwa kwenye kipindi cha Sports HQ cha Radio EFM mapema leo Ijumaa (Julai Mosi).

Mangungu amesema: “Kumekua na maneno mengi sana kuwa, Mwalimu anakuja kwenye timu halafu anakuta maamuzi ya kuleta wachezaji hausiki 100%”

“Niwahakikishie tu kuwa Kocha wetu mpya wa Klabu ya SIMBA, Atashiriki vizuri katika kuchambua wachezaji waliopo sasa, kisha ataona nani abaki na tutafanya usajili pia kwa kumsikiliza na kumshauri pia wakati mwingine”

“Hatuwezi kununua tu wachezaji kwa gharama kubwa na kisha kuwaacha tu hewani, tunataka mashabiki wa simba waridhike na klabu na sio kufanya maamuzi tu kwa kuwa tuna hiyo nafasi.”

“Kocha Zoran Manojlovic atashiriki kwenye usajili kwa asilimia zote ndani ya klabu ya Simba SC.

Tayari Simba SC imeshamtangaza Mshambuliaji kutoka nchini Zambia Moses Phiri, ambaye atakua sehemu ya kikosi chao msimu ujao wa Ligi Kuu na Michuano ya Kimataifa, ambao umepangwa kuanza rasmi mwezi Agosti.

Issa Ndala mali halali Azam FC
Waziri Mkuu aachia madaraka