Madiwani wa Halamshauri ya Manispaa ya Iringa mkoani humo wameipongeza halmashauri hiyo kwa kuendelea kuongoza kitaifa katika ukusanyaji wa mapato kwa kundi la Halmashauri za Manispaa nchini .

Madiwani hao wametoa pongezi hizo mara baada ya taarifa ya Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa, Alex Kimbe kutoa taarifa rasmi katika kikao hicho kuhusu Manispaa ya Iringa kuongoza kwa ukusanyaji wa mapato kwa mwezi Januari .

Diwani wa Kata ya Mwangata, Edward Chengula amesema kuwa ni hatua ya kujipongeza kwa halmashauri hiyo ya Manispaa ya Iringa kuendelea kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato na kuwa kinachoendelea ni uwajibikaji mzuri wa watendaji wa halmashauri hiyo chini ya mkurugenzi wake Hamid Njovu pamoja na madiwani .

”Ushirikiano uliopo ndio ambao umepelekea Halmashauri yetu kuendelea kuwa pamoja na kuwatumikia wananchi kwa nguvu ya umoja bila kuwepo mivutano ya kisiasa, hadi sasa mfano Kata yangu ya Mwangata najivunia kuona watoto waliofaulu kujiunga na elimu ya sekondari wote wanakwenda shule ila pia kuna maendeleo makubwa yanayofanywa katika kata ya Mwangata,”amesema Chengula

Aidha, kwa upande wake Naibu meya wa Manispaa ya Iringa, Joseph Lyata amesema kuwa kuongoza kwa Manispaa hiyo katika ukusanyaji kodi ni ishara nzuri kuwa wananchi wa Manispaa ya Iringa wameitikia wito wa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli ya kila mmoja kulipa kodi kwa maendeleo ya Taifa .

Naye Mbunge wa viti maalum mkoa wa Iringa, Ritta Kabati (CCM) na mbunge wa viti maalum mkoa wa Iringa, Suzana Mgonakulima (Chadema) wamesema kuwa mbali na kuipongeza manispaa yao kwa kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato ila wanapongeza kwa ujenzi wa vyumba vya madarasa ambavyo vimepelekea watoto wote kwenda shule .

 

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Februari 20, 2019
RC Ole Sendeka atajwa mkoani Njombe