Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imebaini upotevu wa zaidi ya shilingi bilioni 10 unaotokana na ukwepaji kodi unaofanywa na makampuni 12 ya wafanyabiashara yanayoweka mabango katika maeneo mbalimbali ya Manispaa hiyo.

Meya wa Manispaa hiyo, Boniface Jacob (Chadema), jana alieleza kuwa manispaa hiyo ilitarajia kupata shilingi bilioni 13 kutokana na mabango yanayokwekwa barabarani, lakini baada ya kufanya upembuzi imebaini kuwa kiasi hicho hakilipwi. Badala yake, wafanyabiashara hao wamelipa shilingi bilioni 2.5 tu.

Kiasi hicho kimepotea kutokana na udanganyifu unaofanywa na wafanyabiashara kuandika kwenye mkataba idadi ndogo ya mabango yanayopatikana kwenye maeneo mbalimbali ya manispaa hiyo.

Alisema kuwa wafanyabiashara hao wanashirikiana na watendaji wasio waaminifu kufanya udanganyifu huo. Alieleza kuwa Manispaa hiyo imeunda timu tatu ambazo zimefanya kazi kubwa na kubaini upotevu huo mkubwa wa fedha.

Alitoa mfano wa kampuni moja ambayo ilipaswa kulipa kodi ya shilingi bilioni 2, lakini ilikwepa kwa kuandika idadi ndogo ya mabango na kulipa kodi ya shilingi milioni 500 tu.

“Tungewatumia watumishi wa ndani kufanya uchunguzi huu ingekula kwetu.Lakini hizi timu tatu zimefanya kazi kubwa, kwa sababu hawa wamiliki wa mabango wanapiga fedha nyingi, ukiwa na bango moja Kinondoni unalipia Sh30 milioni tena kwa dola,” alisema Jacob.

Meya huyo aliwapa siku 7 wafanyabiashara wote waliokwepa kodi kujisalimisha na kulipa kiasi chote cha kodi walizokwepa kutokana na idadi ya mabango waliyonayo.

“Tunahitaji hizi fedha walizokwepa kulipa haraka iwezekanavyo ili tuzipeleke kwenye sekta ya elimu. Najua kuna wengine watazunguka mlango wa nyuma na kwenda ngazi za juu kutafuta huruma, lakini nawaambia huko wanajisumbua bora waje hapa ofisini tena wakiwa na fedha zetu,” alisema Jacob.

Alisema kuwa upotevu huo wa fedha unazigharimu Halmashauri nyingi na kukwamisha mipango mbalimbali yenye maslahi makubwa kwa taifa na maendeleo ya wananchi.

 

 

 

Mimba ya Wema Sepetu yayeyuka, Idris alia kupoteza mapacha
Raia wa India anyooshwa baada ya kuwaita watanzania ‘Nyani’