Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji amesema atakwenda kwenye mkutano wa wanachama wa klabu hiyo Oktoba 23 na kumalizana nao.

Manji amezungumza leo mchana na kusema atakwenda katika mkutano huo ili kujua hatma ya Yanga, pia ya kwake kwa kuwa anataka kupata uhakika wa kila jambo, hivyo bado yuko Yanga.

Taarifa kutoka ndani ya ofisi ya Manji, zimeeleza kwamba ameanza maandalizi ya kujiondoa baada ya kuona kila kitu anachofanya ndani ya Yanga kuna mpango wa kukizuia.

“Nimesikia taarifa za kuondoka kwangu, naomba muelewe kuwa mimi ni binadamu pia. Ninachoshwa na mambo fulani, ninaumizwa moyo na wakati mwingine nakata tamaa.

“Kila ninachofanya kupiga hatua kinazuiwa, lakini wanaozuia hakuna hoja ya msingi wanayoeleza. Inakuwa ni kama kutaka tu kunizuia, tutapiga vipi hatua kwa kubaki palepale?

“Hatma yangu itakuwa Jumapili siku ya mkutano, sitaki kuwaumiza mashabiki na wanachama wa Yanga ambao wameniunga mkono muda wote.

“Najua kuna watu hawataki mabadiliko lakini hawasemi wazi, lakini Wanayanga ndiyo wataamua hatma ya Yanga na suala la ukodishwa, mimi na hatma yangu Yanga, vyote vitajulikana.

“Kuondoka ghafla nitawaumiza Yanga, najua bado wako kwenye mapambano. Angalia leo tuna mechi dhidi ya Mtibwa. Bado tunaendelea kupambana na mambo si mazuri hadi sasa.

“Ushauri wangu waambie Wanayanga kwa tupo pamoja. Tuendelee kupambana kwa ajili ya klabu yetu, lakini Jumapili kwenye mkutano, hatma itajulikana,” alisema.

Kumekuwa na wanaopinga Kampuni ya Yanga Yetu Ltd kukodishwa Yanga kwa miaka 10 lakini tayari ilishaingia mkataba na bodi ya wadhamini wa klabu ya Yanga.

Makubaliano yalifikiwa baada ya mkutano wa dharura wa wanachama ambao asilimia zaidi ya 98 waliliridhia na bodi ya wadhamini inayoongozwa na Mama Fatma Makure ikaanza kufanya kazi ya kushughulikia masuala ya mkataba kisheria hadi uliposainiwa.

Baada ya kusainiwa kwa mkataba huo, ulisambazwa kwenye vyombo vya habari kupitia bodi hiyo ya wadhamini na hapo ndipo mjadala ulipoibuka hasa baada ya Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo (BMT), Mohamed Kiganja kutangaza hawautambui.

Jana, TFF nao kupitia Katibu Mkuu, Mwesigwa Selestine nao wakatangaza kutoutambua mkataba huo.

Chanzo: na Salehjembe

 

 

Video: Mji wa Dodoma lazima upangwe - Majaliwa
Nyerere chimbuko la Ukombozi Afrika