Bondia Manny Pacquiao ametua jana nchini Australia kwa ajili ya pambano kubwa la kihistoria nchini humo, dhidi ya mbabe ambaye hajawahi kushindwa pambano, Jeff Horn. Pambano hilo limebatizwa jina na ‘Battle of Brisbane’, Julai 2.

Pacquiao ambaye ni seneta nchini kwake akishikilia mkanda wa ubingwa wa dunia ambao atautetea kwenye pambano hilo, amepata mapokezi makubwa katika uwanja wa ndege wa Australia. Aliondoka nchini kwao Ufilipino akiagwa kama kiongozi wa ngazi ya juu na paredi ya jeshi.

“Katika miaka yangu yote ya ndondi, sijawahi kuhamasika na kuwa na moto kama ilivyo kwenye pambano hili,” alisema Pacquiao baada ya kufika Australia.

“Timu yangu ina furaha kutokana na maandalizi yangu. Ninatarajia mazuri kwenye hili pambano na nitakuwa narudi nyumbani kama bingwa wa dunia,” aliongeza.

Hata hivyo, mpinzani wake Horn amekuwa akitamba pia kuwa ataweza kumpiga kwa ‘knock out’ Pacquiao kwani anaamini atamnasa na mkono wake wa kulia ambao anaamini hautamuacha salama.

Pambano hilo litakaloshuhudiwa katika uwanja wa mpira wa miguu wa Suncorp, Brisbane nchini Australia na litahudhuriwa na zaidi ya watu 60,000 kwenye uwanja mkubwa wa mpira wa miguu.

Pacquiao amesisitiza kuwa hamchukulii poa Horn kwakuwa anajua ni bondia ambaye ana uwezo mkubwa.

Manji amwangukia JPM, aomba radhi kwa yaliyopita
Vanessa Mdee afunguka kuhusu kupigana chini na Jux