Bondia ambaye pia ni Seneta wa Ufilipino, Manny Pacquiao, leo amerejesha matumaini ya kuendelea kupambana baada ya kumpiga kwa KO, bondia wa Argentina, Lucas Matthysse.

Pacquiao ambaye alionekana kumlemea Matthysse tangu randi ya kwanza ya pambano, akimpiga chini mara mbili, katika raundi ya 3 na ya 5, amekata kiu ya kupata ushindi wa KO tangu mwaka 2009.

Ushindi huo wa Pacquiao umewaondolea mashabiki wake mashaka kuwa huenda bondia huyo angeachana na masumbwi kutokana na umri wake (miaka 39), kwa kuzingatia pia historia ya kushtushwa na kipigo kutoka kwa bondia wa Australia, Jeff Horn kilichozua utata.

Rais wa Ufilipino, Rodrigo Duterte alikuwa katika kiti cha mbele akishuhudia pambano hilo. Alienda nchini Malaysia kwa ajili ya kushuhudia pambano hilo pamoja na kufanya ziara ya kikazi ya siku mbili.

Akizungumza baada ya ushindi huo, Pacquiao amesema kuwa hakutegemea kushinda kwa KO, kwani Matthysse ni mpinzani mgumu na imara.

“Imenishangaza! Matthysse ni mpinzani imara sana na nimemzima kwa KO. Hiyo kwangu ni ziada kutokana na kuwa mvumilivu na kufanya maandalizi kwa bidii,” alisema Pacquiao.

Kwa upande wa Matthysse alisema, “wakati mwingine unashinda na wakati mwingine unashindwa. Leo ilikuwa wakati wangu wa kushindwa, lakini nimepoteza kwa nguli mwenye heshima.”

Kutokana na ushindi huo, Manny Pacquiao ameweka rekodi ya kushinda mara 60, akipoteza mara 7 na kutoa sare mara 2. Imekuwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 15, Manny amepigana bila kuwa na kocha wake, Freddie Roach.

Kadhalika, amebadili rekodi yake na kuwa ameshinda kwa KO 40. Huenda Manny akakamilisha ahadi yake ya kupambana na bondia machachari wa Ukraine anayetajwa kuwa ni bondia bora zaidi duniani kwa uzito wa Welterweight, Vasyl Lomachenko.

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Julai 15, 2018
Video: Wakulima Dakawa wanufaika na kilimo cha umwagiliaji baada ya Serikali kukarabati mindombinu