Bondia Manny Pacquiao ambaye pia ni Seneta nchini Ufilipino amevitembelea vikosi vinavyopambana na magaidi wa kundi la ISIS waliolivamia jiji la Marawi nchini humo kwa wiki kumi hadi sasa.

Pacquiao alitembelea kikosi kilichoko katika eneo la Kusini mwa nchi hiyo majira ya saa tatu asubuhi (kwa saa za Ufilipino) akiwa amevalia sare za kikosi maalum cha jeshi la nchi hiyo ambacho kiliwahi kumtunuku ujumbe wa heshima wa kikosi hicho (honorary member).

Kwa mujibu wa Rappler, Pacquiao aliwatia moyo wanajeshi wanaopambana katika eneo hilo huku akieleza kuwa ana nia ya kujiunga na vikosi hivyo kusaidia mapambano.

“Nataka kujiunga nanyi katika mapambano, mtapenda iwe hivyo. Msirudi nyuma, kwasababu ndivyo ilivyo hata kwenye masumbwi, tuko katika raundi ya 3 lakini ni kama vita imeshakwisha,” Pacquiao anakaririwa na Rappler.

“Nyie ndio mashujaa wa kweli, mimi ni bondia tu. Ninyi mmejitolea maisha yenu kwa nchi yetu. Ninaamini nitarudi tena kuwatembelea baada ya kumaliza mapambano. Lakini kama nitarudi na kukuta bado mnaendelea kupambana basi mimi pia nitaenda huko [kupambana],” aliongeza.

Mapambano hayo yamesababisha zaidi ya watu 400,000 kuyakimbia makazi yao jijini Marawi na maeneo mengine ndani ya Ufilipino.

Vifo vilivyothitishwa na Mamlaka ya usalama nchini humo ni magaidi 630, raia 45 na wanajeshi wa Serikali 114.

Taarifa ya jeshi hilo kwa umma kuhusu ziara ya Pacquiao imeeleza kuwa imeviongezea ari vikosi hivyo.

“Tunaamini vikosi vyetu vilivyo kwenye mapambano vimeongeza nguvu zaidi baada ya kuona kuwa Seneta Pacquiao amevitembelea na kuonesha jinsi anavyoviunga mkono ingawa ana ratiba ngumu,” Luteni Jenerali Galvez amekaririwa katika taarifa ya jeshi hilo.

Magazeti ya Tanzania leo Julai 31, 2017
Video: Simba kwachafuka, Wazee Simba wagomea mabadiliko