Mlinda mlango Manuel Neuer anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha timu ya taifa ya Ujerumani mwishoni mwa juma hili, wakati wa mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Austria.

Mlinda mlango huyo anatarajiwa kurejea uwanjani kwa mara ya kwanza, baada ya miezi tisa kupita, kutokana na majeraha ya mguu yaliyokuwa yakimkabili.

Kocha wa makipa wa timu ya taifa ya Ujerumani Andreas Koepke amethibitisha utayari wa Neuer, baada ya kufanya mazoezi kwa kipindi cha miezi kadhaa, na baadaye kuitwa kwenye timu ya taifa ambayo itakwenda nchini Urusi kutetea taji la Dunia.

“Huo ni mpango,” amesema Koepke akiwaambia waandihi wa habari wakati timu ya taifa ya Ujerumani ikifanya mazoezi jana katika kambi ya Eppan, kaskazini mwa Italia.

“Kila kitu kinakwenda vizuri kwa sasa, na tunaamini ataonyesha uwezo wake katika mchezo wa jumamosi. Hakuna njia ya mkato iliyotumika ili kumuharakisha kurejea uwanjani, tumefuata utaratibu aliopangiwa wa kufanya mazoezi, na kwa sasa Neuer yupo tayari.”

Mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 32, alikiongoza kikosi cha Ujerumani kama nahodha kwa dakika 30, wakati wa mazoezi ya timu hiyo, ilipocheza dhidi ya kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 20 cha nchi hiyo juzi jumatatu, na leo jumatano anatarajiwa kucheza dakika nyingine 30 katika mazoezi ya timu hizo mbili zitakapocheza tena.

Kikosi cha Ujerumani kitaendelea kuwa kambini kaskazini mwa Italia haji Juni 05, siku moja kabla ya kuwasilisha majina 23 ya wachezaji watakaosafiri kuelekea nchini Urusi kwa shughuli ya kutetea taji la Dunia.

Kwa sasa kikosi cha Ujerumani kina wachezaji 27, na kocha Joachim Loew atapunguza majina ya wachezaji wawili na kubaki na kikosi cha wachezaji 25.

Mbali na mchezo wa kirafiki dhidi ya Austria, Ujerumani watacheza mchezo mwingine wa kirafiki dhidi ya Saudi Arabia mjini Leverkusen  Juni 8, ukiwa mchezo wao wa mwisho kabla ya kuanza safari ya kwenda Urisi kukabiliana na timu za kundi F, ambazo ni Sweden, Korea Kusini na Mexico.

Mshike mshike wa fainali za kombe la dunia, unatarajiwa kuanza rasmi Juni 14.

Maajabu 7 ya korosho kwa mwili wa binadamu
Video: Mbowe alia siasa mazishi ya Bilago, Dk. Bashiru arithi mikoba ya Kinana.