Kocha wa makipa wa klabu ya Simba, Milton Nienov, amesema viwango vya makipa wote watatu wa Simba kwa sasa viko juu, tofauti na mwanzo alivyokuja.

Kocha huyo kutoka nchini Brazil ambaye alijiunga na Simba SC mwezi uliopita, amesema makipa wote aliuowakuta kwenye kikosi hicho ni wazuri, lakini alichofanya ni kuwaongezea mbinu ambazo zitawafanya waonekane bora.

Kocha huyo anafanya kazi ya kuwania makipa wa Simba SC  wakiongozwa na chaguo la kwanza Aishi Manula, Beno Kalolanya na Ally Salim.

“Hakijaongezeka kwa Manula tu, au kwa Kakolanya, ila hata kwa Ally, naye ameongezeka kiwango na kama akipata nafasi ataonyesha kile ambacho amekipata,” amesema kocha huyo.

Mashabiki wengi wa soka nchini kwa sasa wameonekana kukoshwa na kiwango cha hali ya juu cha Manula akiwa na Simba SC pamoja na timu ya Taifa, Taifa Stars.

Manula ambaye kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika amecheza michezo minne bila wavu wake kutikiswa, lakini alitia fora kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) zilizomalizika hivi karibuni nchini Cameroon.

Kwa miaka ya hivi karibuni, Manula alikuwa akituhumiwa kushuka kiwango kwa kuruhusu mabao rahisi akiwa kwenye timu ya taifa na hata akiwa na Simba SC.

Na hii ilisababisha hata viongozi wa Simba SC, pamoja na mambo mengine, kubadilisha kocha wa makipa ambaye wakati huo alikuwa Mwarami Mohamed, kabla ya kumtwaa Mbrazil huyo.

Manula hakufungwa kwenye mchezo wa awali kati ya Simba dhidi ya Plateau United, timu yake ikishinda bao 1-0 ugenini na suluhu nyumbani, ikishinda mabao 4-0 nchini Tanzania dhidi ya FC Platinum ya Zimbabwe, na ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya AS Vita ya DR Congo.

Kaze aukubali 'MZIKI' wa Kagera Sugar, Mexime achekelea
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Februari 18, 2021