Wasichana wawili mapacha waliokuwa wanasubiri kufunga ndoa siku moja wametekwa Kusini-Magharibi mwa jimbo la Zamfara nchini Nigeria.

Makamu Mwenyekiti wa eneo hilo, Abubakar Muhammad amekaririwa na BBC akieleza kuwa mapacha hao Hassan na Hussaina Bala Dauran, walikuwa miongoni mwa watu saba waliotekwa wikendi iliyopita katika mji wa Dauran.

“Watu saba, ambao ni wanaume wanne na wanawake watatu walitekwa kati ya Jumamosi na Jumapili,” alisema.

“Watu wengine wawili, mwanaume na mwanamke pia walitekwa katika kijiji cha Birnin Tsaba, huku wengine watatu wakishikiliwa na watekaji katika mji wa Moriki akiwemo kiongozi wa serikali za mitaa,” aliongeza.

Imeelezwa kuwa mapacha hao wenye umri wa miaka 18 walitekwa walipoenda kumuonesha binamu yao nguo zitakazovaliwa kwenye harusi yao itakayofanyika Disemba mwaka huu.

Kwa mujibu wa Muhammad, watekaji hao wamewasiliana na wazazi wa mapacha hao wakidai pesa kama sharti la kuwaachia huru.

Eneo la Zamfara linadaiwa kuwa na changamoto kubwa ya kiusalama ambapo takribani watu 400 wameripotiwa kuuawa mwaka huu. Pia, vitendo vya unyang’anyi, mauaji na utekaji vimeripotiwa kuongezeka.

Vyama saba vya upinzani vyaungana kugombea Urais
Mtangazaji afunga ndoa feki kutoa msaada wa ada chuo kikuu

Comments

comments