Umoja wa Mataifa umesema, mapigano yanayoendelea katika baadhi ya maeneo ya mji wa Tigray nchini Ethiopia yanakwamisha shughuli za upelekaji wa misaada ya kibinadamu huku ripoti zikionesha kuwa mamilioni ya watu wanaelekea kukosa chakula.

Maofisa wa umoja wa Mataifa wameliambia shirika la habari la AFP kuwa, hawakuweza kufikisha misaada kama walivyokubaliana na utawala wa Addis Ababa, hasa kwenye maeneo ambayo yanakaliwa na vikosi vya serikali.

Mwishoni mwa juma lililopita, jeshi liliingia kwenye mji wa Mekele na kutangaza kumalizika rasmi kwa operesheni za kijeshi kwenye mji wa Tigray.

Baadhi ya vyombo vya habari vya kimataifa, vimeripoti kuhusu uwepo wa mapigano kwenye baadhi ya maeneo licha ya kuwa serikali inakanusha kuhusu kuendelea kwa mapigano.

Mamia ya watu wameripotiwa kuuawa katika mji wa Tigray, huku maelfu wengine wakikimbilia nchi jirani ya Sudan kuomba hifadhi.

Viongozi wa TPLF wanaoongoza eneo la Tigray, ambao tayari wamekimbia mji huo wameapa kuendelea na vita kwa kile walichosema ‘hawawezi kuona mji wao unachukuliwa na wavamizi’.

Ivory Coast: Gbagbo arudishiwa hati za usafiri
Askari JWTZ mikononi mwa polisi akituhumiwa kumuua mkewe.