Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Omar Hassan Omar, amesema jumla ya timu tisa zitashiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi 2021, inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi kisiwani Unguja kati ya Januari Mosi ama 3.

Omar amesema timu zinazotarajiwa kushiriki michuano hiyo kutoka Tanzania Bara ni Simba, Young Africans, Azam FC, Namungo FC na mabingwa watetezi Mtibwa Sugar, huku kwa upande wa visiwani Zanzibar ni Mlandege na Malindi pamoja na mbili kutoka Ligi Daraja la Kwanza Kanda ya Pemba ambazo ni Jamhuri FC na Chipukizi.

Amesema tayari Young Africans imethibitisha kushiriki michuano hiyo, lakini kwa upande wa Simba na Namungo licha ya kukubali, zimesema ushiriki wao utategemeana na ratiba ya Ligi Kuu Bara na ile ya mechi za kimataifa, Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika itakavyokuwa.

Simba inaiwakilisha nchi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Namungo pia ikiwa na kibarua cha kuipeperusha bendera ya Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho.

Katika hatua nyingine, Omar alitaja kamati itakayosimamia mashindano hayo ambapo Mwenyekiti atakuwa ni Khamis Abdallah Said, Katibu ni Aiman Duwe na Naibu Katibu akimtangaza kuwa ni Suleiman Pandu.

Kwa upande wa Wajumbe wa Kamati ya Mashindano ya Kombe la Mapinduzi, aliwataja kuwa ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Khamis Mussa Omar, Katibu Mkuu Wizara ya Michezo Muungano, Dk. Hassan Abbas, Mratibu wa Shughuli za Serikali (SMZ), Issa Mlingoti na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini, Omar Singo.

Wajumbe Wengine ni Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Neema Msika, Ambar Sharif, Meneja wa Uwanja wa Amaan na Mau, Abdulhamin Mohamed Juma, Ofisa Mdhamini Wizara ya Habari, Fatma Hamad Rajab, Rais wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), Seif Kombo Pandu, Makamu wa Rais wa ZFF, Salum Ubwa, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Zanzibar, Chande Omar na Juma Mmanga.

Lwandamina: Nitasajili dirisha dogo
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Desemba 16, 2020