KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imepangwa Kundi B kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi, inayotarajia kufanyika ndani ya Uwanja wa Amaan, Visiwani Zanzibar kuanzia Desemba 30 hadi Januari 13 mwakani.

Azam FC ambayo iliishia hatua ya makundi mwaka huu, imepangwa pamoja na Yanga kwa mara ya pili mfululizo huku timu nyingine zikiwa ni Jamhuri na Zimamoto, zote za visiwani humo.

Timu hiyo pia iliwahi kupangwa na Yanga kwenye hatua hiyo mwaka 2012 na kuifunga mabao 3-0, ushindi ulioitupa nje ya michuano Yanga, kabla ya Azam FC kutinga nusu fainali na kwenda kutwaa ubingwa mbele ya Jamhuri kwa kuwachapa 3-1.

Mabingwa hao mara mbili wa michuano hiyo (2012, 2013), wataanza kufungua dimba Januari 2 kwa kuchuana na Zimamoto saa 10.15 jioni kabla ya kuvaana na Jamhuri Januari 4 saa 2.15 usiku.

Wakazi wa visiwani humo wanatarajia kushuhudia mpambano wa aina yake Januari 7, pale mahasimu Azam FC na Yanga watakapochuana kwenye mchezo wa kufunga hatua ya makundi utakaofanyika saa 2.15 usiku.

Washindi wawili wa juu kwenye kundi hilo wanatarajia kutinga hatua ya nusu fainali na kuungana na timu nyingine mbili zilizofanya vizuri Kundi A, linaloundwa na timu za Simba, Taifa ya Jang’ombe, Jang’ombe Boys, KVZ na mabingwa watetezi wa michuano hiyo, URA, ambao waalikwa kutoka Uganda.

Michuano ya mwaka huu mwanzoni, Azam FC ilishindwa kuingia hatua ya nusu fainali baada ya kulazimishwa sare mechi mbili dhidi ya Yanga (1-1), Mtibwa Sugar (1-1) na kupoteza dhidi ya Mafunzo mabao 2-1.

Mpina afanya ziara ya kushtukiza Bandari ya Dar es salaam
Ridhiwani aomba waajiri kutoa nafasi kwa vijana, akemea dhana potofu...