Rais wa Guinea, Alpha Condé yuko matatani baada ya kusambaa kwa kipande cha video kikimuonesha amezungukwa na wanajeshi ambao wamedai kuwa wamepindua Serikali yake.

Jana, kiongozi wa vikosi vya makomando wa Guinea alitangaza kupitia Televisheni ya Taifa ya nchi hiyo kuwa wamefanya mapinduzi halisi na wanamshikilia Rais Conde.

Hatua hiyo imekuja saa chache baada ya kusikika milio ya risasi karibu na Ikulu, katika Mji Mkuu wa Conakry.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres pamoja na Umoja wa Afrika wamelaani kitendo cha mapinduzi hayo, na kuwataka wanajeshi hao kumuachia mara moja Rais Conde.

Mapinduzi hayo yamefanyika ikiwa ni takriban mwaka mmoja baada ya Rais huyo kushinda uchaguzi kwa mara ya tatu baada ya kubadili Katiba. Mabadiliko ya Katiba yalimfanya kubaki madarakani zaidi ya awamu mbili zilizokuwa zimewekwa awali. Guinea ambayo ni nchi iliyobarikiwa rasilimali nyingi asilia, ni miongoni mwa nchi masikini zaidi duniani

Dunia yalaani Mapinduzi Guinea
Wabunge wajengewa uelewa kuhusu Uviko 19