Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kutoa umuhimu wa kuziimarisha huduma za mama na mtoto ili kuhakikisha kwamba vifo vinavyotokana na uzazi vinapungua na kumalizika nchini.

Makamu wa Rais ameyasema hayo katika hafla ya Uwekaji wa Jiwe la Msingi wa Jengo la huduma za Mama na Mtoto katika Hospitali ya Kivunge wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazinin Unguja ikiwa ni shamra shamra za kutimiza miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema mara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyoongozwa na Jemedari Mkuu Marehemu Mzee Abeid Amani Karume serikali ilitangaza matibabu bure kwa wananchi wote bila ya ubaguzi kwa lengo la kujenga msingi wa uwapatikanaji wa huduma za afya nchini.

Mama Samia ameeleza kuwa sera hiyo ilitia mkazo zaidi katika kutoa kinga hivyo serikali imeweza kusambaza huduma ya afya karibu na wananchi ili kuondosha upungufu wa kwenda masafa marefu kufuata huduma hiyo ambapo kwa sasa takriban vituo 180 vimejengwa ikilinganishwa na mwaka 1964 ambapo vilikuwepo 32.

Makamu huyo wa Rais amefahamisha kuwa kujengwa kwa jengo hilo la huduma ya mama na mtoto katika Mkoa huo litasaidia kupunguza vifo vya wanawake na watoto wakati wa uzazi pamoja na kupunguza msongamano wa wazazi na wagonjwa kupelekwa Hospitali ya Mnazi mmoja.

Aidha amewataka wafanyakazi wa hospitali hiyo kutoa ushirikiano na upendo katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa ili kuweza kutoa huduma nzuri na maendeleo katika sekta hiyo

“Natoa wito kwenu watoa huduma za Afya, Madaktari, wauguzi na wataalamu wa fani mbalimbali za afya mnaotoa huduma katika Hospitali hii, mfanye kazi zenu huku mkijua kwamba Mungu aliwateuwa nyinyi kuhudumia wanadamu wenzenu, hivyo basi timizeni majukumu yenu kila mmoja kwa fani yake mkiwa na hofu kwa Mungu”, ameeleza Mama Samia.

Iran yakiri kutungua ndege ya abiria ya Ukraine, Rais atoa tamko
Tanzania kushuhudia kupatwa kwa mwezi usiku wa leo