Serikali nchini, inatarajia kufanya mapitio ili kupunguza gharama za kusafisha figo, ambazo zinalalamikiwa na Wananchi walio wengi kuwa ni za juu na hivyo kushindwa kuzimudu na kupelekea wengi wao kupata athari au kupoteza maisha.

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel ameyasema hayo Bungeni jijini Dodoma, na kusema kwa sasa bili za matibabu ya kusafisha damu ni Shilingi laki tisa kiasi ambacho ni kikubwa kwa watu wa kipato cha chini ambao hushindwa kumudu.

Ahadi ya mapitio hayo, ilitokana na swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mariam Kisangi aliyetaka kujua ni mpango gani wa serikali katika kuwasaidia wagonjwa wa figo kupata matibabu ya kusafisha figo kwa gharama nafuu.

Katika swali la nyongeza la Mbunge Kisangi, aliomba kupunguzwa kwa bili hizo, na kutaka wagonjwa wanaotumia bima ya afya wajumuishwe katika matibabu hayo ili iwe rahisi kwao kupata tiba.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri huyo amesema mkakati wa Serikali katika kupunguza gharama ni kununua vifaa tiba na vitendanishi moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji hali ambayo itafanikisha kazi husika na kwamba muswada wa sheria ya Bima ya Afya kwa wote utakapokamilika, ni suluhisho la kudumu.

“Sera ya Afya ya nchi inaelekeza kuwa hakuna Mtanzania anayepaswa kufa kwa kukosa fedha za matibabu kwahiyo Serikali imekuwa ikiwasamehe wale wote ambao wanakidhi vigezo na hawana uwezo wa kifedha,” alisema Naibu Waziri.

Kuhusu mpango wa kupunguza bili za matibabu, Serikali imesema inafikiria kushusha kiwango hicho hadi Shilingi elfu 50 kwa mgonjwa mmoja.

FIFA yaiadhibu Biashara United Mara
Waliotekwa na Boko Haram wapatikana wakiwa na watoto