Imeelezwa kuwa Kila mwaka watu 20 hupoteza maisha kutokana na kichaa cha mbwa mkoani Mara huku kati ya watu 1,000 na 2,500 wakiwa katika hatari ya kuambukizwa ugojwa huo.

Kutokana na tatizo hilo, mkakati wa kutokomeza kichaa cha mbwa kwa binadamu na kuokoa maisha ya watu umezinduliwa na taasisi ya afya Ifakara (IHI) kwa ushirikiano na shirika la kimataifa la Global health.

Taasisi hiyo imeendesha mafunzo ya siku tatu kwa wenyeviti 54 wa vijiji kutoka kata 12 za wilaya ya Tarime ili kuwajengea uwezo wa kukabiliana na ugonjwa huo na kudhibiti maambukizo mapya.

Kwa mujibu wa mratibu wa mradi huo, Dkt. Ahmed Lugelo, amesema utakuwa na miaka mitatu kuanzia mwaka huu hadi 2023 ukilenga pia kuhakikisha watu wanaong’atwa na mbwa wanapata tiba haraka na mwisho kutoa chanjo kwa mbwa wote maeneo hayo.

Akizungumza wakati wa utoaji wa chanjo ya mfano ambayo mbwa zaidi ya 200 walichanjwa katika kijiji cha Kewamamba, Dkt. Lugelo amesema maofisa ugani watawezeshwa mafunzo ya mfumo rasmi wa kutumia simu za mkononi kuratibu na kutoa taarifa za kesi za kichaa cha mbwa.

” Njia pekee ya kuepuka ugonjwa wa kichaa cha mbwa ni kupitia kuchanjwa mbwa ama kwa njia ya haraka kuchanjwa baada ya kung’atwa” amesema Dkt. Lugelo.

Ofisa Mifugo wa halmashauri ya wilaya ya Trime, Dkt. Peter Nyanja amesema jitihada zinahitajika kuhakikisha ugonjwa wa kichaa cha mbwa unaangamizwa kabisa si tu eneo la wilayani bali maeneo mbalimbali nchini ili kutimiza lengo la kuutokomeza kabisa ifikapo 2030.

 

Zimbabwe yathibitisha kisa cha kwanza mgonjwa wa Corona
Wachezaji wa kigeni wawekwa mtegoni