Nyota bora wa soka wa muda wote ambaye pia alikuwa mshambuliaji wa kikosi cha taifa cha Argentina, Diego Maradona amejitolea kukinoa tena kikosi cha timu hiyo bila malipo yoyote.

Maradona aliweka wazi mpango huo siku moja baada ya Argentina kuondolewa kwenye fainali za kombe la dunia zinazoendelea nchini Urusi, kwa kipigo cha 4-3 dhidi ya Ufaransa, wikendi iliyopita.

Nguli huyo wa Soka aliulizwa na kituo cha runinga cha Venezuela kama angetamani kukinoa tena kikosi hicho ingawa kocha Jorge Sampaoli ana mkataba wa kazi hiyo hadi mwaka 2022.

“Ndiyo, nitapenda kufanya hivyo tena bure. Sitaomba kulipwa chochote kwa kazi hiyo,” alisema Maradona.

“Watu wanadhani nina furaha lakini moyo wangu ni mzito. Ninajisikia kama kila kitu tulichokuwa tunajenga kwa jitihada kubwa tumekiharibu kirahisi,” aliongeza.

Maradona ameendelea kuwa mjadala kwenye fainali za kombe la dunia huku ikikumbukwa pia kwa jaribio lake la kuifanikisha Argentina kunyakua kikombe hicho lilikwama mwaka 2010 akiwa kocha, lakini kikosi hicho kilichapwa na Ujerumani 4-0.

Aliteka vichwa vya habari kwa matukio yake aliyofanya wakati akiishangilia Argentina hivi karibuni ikiwa ni pamoja na kuonesha ishara za matusi na baadaye kupewa onyo na Shirikisho la Soka Duniani (Fifa).

Aidha, amejikuta akipatiwa matibabu ya dharura alipokuwa katika harakati za kushangilia baada ya kukumbwa na tatizo la presha.

TRA yakanusha 'Whatsapp' kuanza kulipiwa kodi
Utaratibu wa kuaga mwili wa Prof. Maji Marefu wapangwa