Viongozi wa Korea Kaskazini na Kusini wamekutana Jijini Pyongyang, Korea Kaskazini na kujadiliana kuhusu kuondoa silaha za nyuklia kwenye rasi ya Korea na masuala mengine ambayo yamekuwa kiini cha mzozo baina yao.

Rais Moon Jae-in wa Korea Kusini aliwasili Pyongyang kwa mkutano huo wa tatu kwa mwaka huu na Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong un.

Aidha, kabla ya kuanza kwa mkutano wao wa kilele Rais wa Korea Kusini na mwenzake wa Kaskazini walitumia gari la pamoja kukatisha katikati ya mji mkuu wa Korea Kaskazini, Pyongyang ambapo maelfu ya raia waliojipanga barabarani huku wakiwashangalia.

Shirika la habari la Korea Kaskazini limenukuu matamshi ya viongozi waandamizi nchini humo kuwa mkutano huo unatoa nafasi ya kuharakisha ushirikiano wa kimaendeleo baina ya Korea mbili ambayo yatatengeneza historia mpya.

Hata hivyo, Moon ambaye alifanya juhudi za kuwa mpatanishi katika mazungumzo kuhusu silaha za nyuklia kati ya Marekani na Korea Kaskazini amesema kuwa watatafuta suluhu ya kudumu wakati wa mkutano huo wa siku tatu.

 

Video: Zifahamu nchi 5 zenye wanawake warembo barani Afrika
Ndugulile: Majibu ya Malaria, U.T.I, Typhoid mengi siyo kweli