Rais wa Venezuela, Nicolás Maduro amesema kuwa Marekani imepanga njama ya kumuua na kupindua serikali yake.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema kuwa mshauri wa usalama wa Taifa wa Marekani, John Bolton anahusika moja kwa moja na njama hiyo japo hakutoa ushahidi wowote kuthibitisha madai hayo.

Aidha, mapema wiki hii maafisa wakuu wa Urusi na Marekani walijibizana baada ya ndege mbili kubwa za kuangusha mabomu za Urusi kutua nchini Venezuela, taifa linalopatikana Amerika Kusini.

“John Bolton amepewa jukumu la kupanga namna ya kuniangamiza, kuleta vikosi vya kigeni na kubuni serikali ya mpito nchini Venezuela, Watu wa Venezuela wanajiandaa kukabiliana na hatua hiyo kwa usaidizi wa mataifa rafiki zake,” amesema rais Maduro katika ikulu ya Miraflores

Aidha, Marekani imekuwa ikikwazika na uhusiano wa karibu wa serikali ya Maduro na Urusi, Uchina na mataifa mengine ambayo yanatofautiana na utawala wa Trump.

Hata hivyo, mashirika kadhaa ya kigeni nchini Venezuela ikiwa ni pamoja na Kellogg na Clorox, yamefunga shughuli zao kutokana na mzozo wa kiuchumi na vikwazo vya Marekani.

 

Ole wake kiongozi wa dini atakaye hubiri Siasa- Lugola
Makonda afuta likizo kwa wakuu wa idara za afya