Marekani imesema kuwa itafikiria kutumia nguvu za kijeshi kukomesha vitendo vya Korea Kaskazini kama italazimika kufanya hivyo.

Tamko hilo la Marekani limetolewa na Balozi wa Marekani, Nikki Haley kufuatia hatua za Korea Kaskazini kufyatua kombora jingine Jumanne, ikiwa ni mfululizo wa vitendo vyake vya kufanyia majaribio silaha zake.

Haley alisema kuwa wakati Marekani inafikiria kuhusu hatua hizo za kijeshi kama italazimika, suala la kuidhibiti zaidi Korea Kaskazini litajadiliwa katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hivi karibuni.

Aliongeza kuwa pamoja na mambo mengine, itaongeza zaidi vikwazo vya kibiashara dhidi ya taifa hilo ambalo limeonekana kuwa sikio la kufa mbele ya makatazo yake.

Aidha, Haley alisema kuwa Marekani itasitisha biashara kati yake na nchi ambazo zinaendelea kufanya biashara na Korea Kaskazini, kinyume na makubaliano ya Umoja wa Mataifa.

“Tutaangalia kwa jicho la karibu nchi yoyote ambayo itaendelea kufanya biashara na taifa hili korofi,” Haley anakaririwa.

Saa chache baada ya kuzungumza hayo, Marekani na Korea Kusini kwa pamoja zilifyatua makombora kadhaa baharini eneo la Japan.

Hata hivyo, Pyongyang imesema kuwa itakubali kufanya majadiliano endapo Marekani itasitisha sera zake ‘kandamizi’ dhidi ya Korea Kaskazini.

China na Urusi wamepinga vikali hatua za kijeshi dhidi ya Korea Kaskazini, ingawa wiki hii walitoa tamko la kulaani majaribio ya makombora yanayofanywa na nchi hiyo.

Bunge la 11 lawapiga kitanzi watumishi Serikalini
JAY-Z afunguka, mama yake kuwa mpenzi wa jinsia moja