Marekani imesema kuwa imesitisha ufadhili kwa Shirika la Umoja wa Mataifa linalotoa misaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA, hatua inayotishia kuzidisha mzozo kati ya Palestina na utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump.

Msemaji wa Rais wa Palestina, Mahmoud Abbas amelaani uamuzi huo wa Marekani ambao ameutaja kama hatua ya kuwadunisha Wapalestina na inayoendana kinyume na maazimio ya Umoja wa Mataifa.

Aidha, kwa upande wake msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani, Heather Nauert amesema kuwa operesheni na muundo wa shirika hilo la UNRWA una mapungufu makubwa na baada ya tathmini ya kina, Marekani imeamua kusitisha ufadhili.

Marekani huchangia karibu asilimia 30 ya bajeti ya shirika hilo ambalo husaidia kutoa huduma ya afya, elimu na huduma nyingine kwa wapalestina takriban milioni 5 katika ukanda wa Gaza, ukingo wa Magharibi mwa Jordan, Syria na Lebanon.

Wengi wa wakimbizi hao ni watu waliokimbia vita vya mwaka 1948 ambavyo vilipelekea kuundwa kwa taifa la Israel ambalo limekuwa katika mgogoro na nchi za mashariki ya kati.

Hata hivyo, Rais wa Marekani, Donald Trump na maafisa wa utawala wake wamesema kuwa wanataka kuboresha maisha ya Wapalestina na pia kuyafufua mazungumzo ya kutafuta amani kati ya Israel na Palestina.

 

Video: Majimbo yote 264 ya Tanzania yatajengwa vyoo- Naibu Spika Dkt. Tulia Ackson
Bobi Wine aruhusiwa kuondoka Uganda