Ikulu ya Marekani imetoa tamko rasmi linalomhusisha moja kwa moja Rais wa Urusi, Vladmir Putin na udukuzi uliolenga kuingilia uchaguzi wa Marekani uliofanyika mwaka huu.

Mshauri wa Rais Barack Obama, Ben Rhodes aliwaambia waandishi wa habari kuwa uchunguzi wao umebaini kuwa kutokana na mfumo wa utawala wa Putin, ni lazima alikuwa akifahamu kwa karibu mpango wa udukuzi wa mifumo ya kompyuta iliyokuwa ikitumika katika kukamilisha uchaguzi huo.

“Kila tunachofahamu kuhusu ufanyaji kazi wa Urusi na namna ambavyo Putin amekuwa akiidhibiti Serikali yake, tunajua kuwa unapozungumzia udukuzi mkubwa na nyeti kama huu, tunazungumzia ngazi ya juu zaidi ya Serikali,” alisema Rhodes.

“Na kwa uhakika, Vladimir Putin ndiye mhusika rasmi wa vitendo vya Serikali ya Urusi,” aliongeza.

Baadhi ya wanaharakati na wafuasi wa aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Democratic, Hillary Clinton wamekuwa wakisisitiza kurudiwa kwa uhesabuji wa kura katika majimbo matatu muhimu yaliyompa ushindi Donald Trump (Republican), huku wakihusisha na udukuzi wa Urusi kuwa huenda ulimsaidia mfanyabiashara huyo kushinda.

Rais Obama aliamuru kufanyika kwa uchunguzi wa kina kuhusu tuhuma za udukuzi wa Urusi kwenye uchaguzi huo na kwamba apewe ripoti kabla ya kumaliza muda wake Januari 20 mwakani.

Polepole abainisha mkakati wake mkuu ndani ya CCM
Mnyama Afunga Safari, Awafuata Ndanda FC