Wakala wa mshambuliaji kutoka nchini Ujerumani na klabu ya Fiorentina ya nchini Italia, Mario Gomez amekanusha taarifa za mchezaji wake kukamilisha mpango wa kujiunga na klabu ya Besiktas ya nchini Uturuki.

Uli Ferber, wakala wa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 30, amesema taarifa zilizochapishwa na baadhi ya vyombo vya habari nchini Ujerumani mwishoni mwa juma lililopita kuhusu uhamisho wa Gomez hazikuwa na ukweli.

Amesema Gomez yupo katika mipango ya kutaka kubadilisha mazingira ya soka lake na huenda akaelekea Uturuki lakini bado makubaliano ya uhamisho wake kutoka Fiorentina kuelekea Besiktas hayajaafikiwa.

Vyombo vya habari vya nchini Ujerumani mwishoni mwa juma lililopita vililiripoti kwamba, Gomez, amekamilisha hatua za kusajiliwa na klabu ya Besiktas kwa ada ya uhamisho wa paund million 6 sanjari na kusaini mkataba wa miaka mitatu.

Gomez alijiunga na klabu ya Fiorentina mwaka 2013, akitokea FC Bayern Munich, na amekuwa akikabiliwa na mazingira magumu ya kucheza kama alivyozoeleka tangu alipoelekea nchini Italia, kwani mpaka sasa ameshaifungia Viola mabao saba kwenye ligi ya Serie A.

Endapo Gomez atakamilisha mpango wa kuelekea nchini Uturuki, atajiunga na magwiji wengine waliosajiliwa na klabu za nchini humo kama Lukas Podolski aliyejiunga na Galatasaray, Robin van Persie pamoja na Luis Nani waliojiunga na Fenerbahce.

Chelsea Yanawa Mikono Usajili wa Pogba
Ronaldinho Gaucho Awaomba Radhi Mashabiki