Serikali Ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kupitia Wizari Wa Habari, Utamaduni, Utalii Na Michezo imewataka wadau wa soka visiwani humo kukubali kwenda sambamba na mabadiliko waliyonayo kwa sasa, baada ya kukubaliwa kuwa wanachama wa kudumu wa shirikisho la soka barani Afrika CAF.

Waziri Wa Habari, Utamaduni, Utalii Na Michezo Zanzibar Rashid Alli Juma amezungumza na Dar24 na kusema tayari wameshawataka wadau wa michezo visiwani Zanzibar kuwa makini na kufuata taratibu za kikatiba na kuachana na mambo ambayo huenda yakawa chanzo cha kufungiwa na CAF.

Amesema serikali imeamua kutoa tahadhari hiyo, kufuatia mazoea ya baadhi ya wadau kuvunja katiba ya chama cha soka visiwani humo ZFA kwa makusudi, kwa lengo la kutetea maslahi yao binafsi.

“Ni kweli migogoro wa kisoka ilikuwepo visiwani Zanzibar, lakini kwa sasa tumeamuru imalizwe ili kupisha mabadiliko ambayo hayana budi kufanywa kwa sasa, dhumuni letu ni kutengeneza mazingira mazuri ya mchezo huo kuchezwa kwa amani na utulivu.”

“Hatutofumbia macho suala lolote ambalo litakua na viashiria vya malumbano katika soka, kwa sababu kuna haja kwa viongozi na wadau wa soka visiwani Zanzibar kukaa chini na kumaliza mambo yao ndani kwa ndani, haipendezi watu kukimbilia mahakamani na kufungua kesi, wakati kuna katiba inayowaongoza.” Amesema Waziri Rashid.

Katika hatua nyingine Waziri Wa Habari, Utamaduni, Utalii Na Michezo Zanzibar Rashid Alli Juma amesema wanaamini wadau wa soka visiwani Zanzibar watakuwa amejifunza mambo mengi kutoka Tanzania bara, ambapo kwa sasa kuna uelewa mkubwa kwa wanachama wa TFF kufuata katiba za CAF na FIFA.

Majaliwa: Serikali itaendelea kuwawezesha vijana kiuchumi
Live: Yanayojiri Bungeni Dodoma